Like Us On Facebook

WANAFUNZI WAANDAMANA KWA KUKOSA MIKOPO ELIMU YA JUU




                   ZAIDI ya wanafunzi 50 waliochaguliwa kujiunga  katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu, jana waliandamana kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa lengo la kukutana na Waziri Shukuru Kawambwa, baada ya kukosa mikopo.
 
Wakizungumza na mwandishi wetu, wanafunzi hao walisema zaidi ya wanafunzi 200  wenye sifa za kupewa mikopo ya elimu na Bodi ya Mikopo (HELBS), wamenyimwa bila maelezo.
 
Walisema kuwa tangu mwisho wa wiki wamekuwa wakihangaika kujua sababu za kutopewa mikopo kutoka katika bodi hiyo bila mafanikio.
Mwanafunzi Ayoub Suleiman aliyechaguliwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema kuwa wameamua kumfuata Waziri Kawambwa ili wajue ni kwa nini hawajapewa mikopo hiyo.
 
Alisema majibu ya wanafunzi walioomba mikopo hiyo yalitoka Septemba 27 mwaka huu, miongoni mwao hawakuwepo kwa maelezo kuwa bajeti imekwisha.
“Waliotupa majibu haya ni wafanyakazi wa mapokezi na walinzi pale bodi ya mikopo, sio wahusika wenyewe kwa kuwa kila tulipoomba kukutana na mkurugenzi, hatukupata nafasi hiyo,” alisema Suleiman.
 
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Godwin Uledi, alisema kuwa juzi waliwashuhudia baadhi ya wazazi wakiwa na suti  na magari ya kifahari wakifika kwenye ofisi za bodi hiyo na watoto wao, na kuingia moja kwa moja kuonana na watendaji, walipotoka walikuwa wakitabasamu, hali iliyoonyesha kuwa wamefanikiwa.
 
Alisema, wanataka wapewe sababu kwa nini hawajapewa mikopo ilhali wenzao wenye vigezo kama vyao wamepata?
 
“Taasisi ya vyuo vikuu nchini ‘TCU’ ilitoa mwongozo kuwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu wakiomba vitivo vya elimu, uhandisi, udaktari, kilimo na sayansi watapata kipaumbele katika mikopo, hivyo nasi tulifuata mwongozo huo ili tupewe mikopo lakini hatujafanikiwa.
 
“Isingekuwa tunahitaji mikopo hii tungeomba katika maeneo mengine ambayo tulikuwa tukikidhi vigezo. Tumeomba katika vitivo hivi ili tupate mikopo,” alisema.
 
Kwa upande wake mwanafunzi aliyechaguliwa katika Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, Revocatus Baltazary, alisema kuwa wamefungua chuo tokea Septemba 18, lakini ameshindwa kuripoti kutokana na wazazi wake kuwa na kipato cha chini.
 
“Sasa sina hata kianzio cha kwendea huko, kwa kuwa wazazi wangu hawana uwezo nitakwendaje?,” alihoji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Ntambi Bunyazu, alisema kuwa wizara imewasiliana na bodi ya mikopo, kwamba wanafunzi hao warudi kule wakapewe maelezo zaidi kwa kuwa kila mmoja ana tatizo lake.
 
Hadi mwandishi wetu  anaondoka katika maeneo hayo, wanafunzi hao waliambiwa waorodheshe tena majina ili wizara iyapeleke HELBS, baada ya wiki moja watakuwa wamepata majibu.
 
Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HELBS, Cosmas Mwaisobya, kwa ajili ya ufafanuzi wa suala hilo, ziligonga mwamba baada ya simu yake ya kiganjani kuita kwa muda mrefu bila majibu.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari