MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), jana alitikisa Jiji la Arusha baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumfutia kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili.
Lema alidaiwa kutoa kauli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alienda kwenye Chuo cha Uhasibu Arusha kama anaenda kwenye sherehe za kuaga mtoto wa kike “send off”.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Devota Msofe baada ya wakili wa serikali, Eliananyi Njiro, kutumia kifungu cha 20 kifungu kidogo cha 1 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kuliondoa shauri hilo ambalo lilikuwa lianze kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo. Upande wa serikali ulipanga kuleta mashahidi tisa.
Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliofurika mahakamani hapo kusikiliza mwenendo wa kesi hiyo waliupokea uamuzi huo kwa shangwe kubwa.
Akizungumza nje ya mahakama mara baada ya uamuzi huo, Lema alisema kuwa alikuwa anajua shauri hilo ni la kutengenezwa ndiyo maana mashahidi wengi walikuwa ni polisi.
“Ni kama nimeshinda kesi, na Mungu ameendelea kutupigania, na tutaendelea kupambana kutafuta haki bila hofu maana miili yetu na nafsi zetu zimeishapoteza maumivu kwa sababu ya mateso yaliyojaa uongo na hila. “Tutaendelea na kelele zetu za kupigania haki bila kurudi nyuma huku uvumilivu ukiwa nguzo yetu kubwa,” alisema Lema.
Hata hivyo, alikiri kutamka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo alienda Chuo cha Uhasibu kama anaeenda kwenye “send-off” kwani yeye ndiye alimpigia simu akimtaka afike kusikiliza kero za wanachuo, lakini hakulipa uzito unaostahili suala hilo hasa ikizingatiwa kuwa pale kuna mwanachuo alikuwa amepoteza maisha.
Lema alisema kuwa wanaweza kuwa wamemfutia kesi hiyo ili kesho wamfungulie nyingine jambo alilodai kuwa yuko tayari kwani anaelewa kuwa lengo ni kutaka kumuogopesha ili aache kuwatetea wananchi kitu alichodai kuwa hawatafanikiwa kwani tayari ana ganzi mwilini mwake, hivyo haogopi kufa, kesi wala kufungwa.
Kwa upande wake wakili wa Lema, Method Kimomogoro alisema kuwa ni vema kama serikali ingeamua kutumia busara ya kuona hakuna kesi toka awali, hivyo wasingefungua kabisa shauri hilo lililopoteza muda wa mahakama na mteja wake, kwani hata maelezo ya kesi yalionyesha dhahiri hakukuwa na kosa la uchochezi.
Alisema kuwa sheria inaruhusu kumfurahia, kumkejeli au kumzomea mtu, ndiyo maana hata bungeni wanaonekana waheshimiwa wakizomeana na kurushiana vijembe, na akadai hata kauli iliyodaiwa kutolewa na Lema dhidi ya mkuu wa mkoa ilikuwa kijembe tu.
Kimomogoro alilitaka Jeshi la Polisi kutenda kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku akiwataka warudi kwenye hoja ya msingi na wawaeleze wananchi endapo wameshawakamata waliohusika na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo Aprili 24, mwaka huu, mshtakiwa Lema akiwa eneo la Freedom Square ndani ya Chuo cha Uhasibu, alitoa maneno ya uchochezi yaliyosababisha uvunjifu wa amani.
Maneno hayo yanayodaiwa kutamkwa ni kinyume na kifungu cha 390 sura ya 35 cha sheria ya kanuni ya adhabu, marejeo ya mwaka 2002 .
“RC anakuja (Chuo cha Uhasibu) kama anaenda kwenye send-off, hajui chuo kilipo wala mauaji ya mwanafunzi wa chuo hicho... (RC) Ameshindwa hata kuwapa (wanafunzi) pole kwa kufiwa na amesema hawezi kuongea na wanafunzi wasio na nidhamu.” Yalinukuliwa baadhi ya maneno yaliyodaiwa kuwa yalitamkwa na Lema.
Kauli hizo zinadaiwa zilipandisha hasira za wanafunzi ambao walianza kumrushia mawe na chupa Mkuu wa Mkoa, Mulongo alipokuwa akiwahutubia kuhusiana na tukio la kifo cha mwanafunzi, Henry Koga kilichotokea Aprili 23, mwaka huu.