WIKI
iliyopita, tasnia ya habari na Watanzania walipatwa na mshtuko baada ya
serikali kuamua kuyafungia magazeti ya kila siku ya Mwananchi na
Mtanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa siku 14, na Mtanzania siku 90 sawa na miezi mitatu.
Mfukunyuku nimelazimika kulifukua hili
ambalo linakumbusha kidonda au kovu lisilopona baada ya ubabe huo
kutumika na kulipeleka kifungo kisicho na ukomo gazeti la Mwanahalisi
ambalo sasa limetimiza mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu kufungiwa.
Ni hukumu mbaya ambayo haipaswi kujadiliwa kutokana na ukweli kuwa kifungo chochote ni lazima kiwe na ukomo.
Pamoja na kuwa ubabe huo umepigiwa
kelele na makundi mengi yakilaumu hatua iliyochukuliwa na serikali dhidi
ya vyombo vya habari vinavyoonekana kuwa mwiba kwa upande wake, lakini
hilo haliwezi kufanikisha kamwe Watanzania kukosa habari.
Sheria mbovu na ulevi wa madaraka
vinaweza kuwa chanzo cha vyombo vingi vya habari kuchukuliwa hatua,
iwapo hatutakuwa tayari kupinga jambo hilo.
Ingawa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe amewasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi bungeni ili
kufuta sheria ya magazeti ya mwaka 1976 bado harakati zinahitajika
katika hilo.
Sheria hiyo inampa madaraka Waziri wa
Habari kuamua anapojisikia kufungia chombo chochote huku yeye akiwa
ndiye mahakama na hakimu. Ni sheria mbovu isiyofaa hata kusomwa mbele za
watu.
Serikali inakosea na inapokosea ni
lazima ielezwe. Katiba tunayojaribu kuitengeneza upya inasema wazi kuwa
kuna uhuru wa kutoa maoni. Ni uhuru upi huo tunaouzungumza ikiwa kuna
kuminya uhuru wa habari?
Halafu serikali inapokuja na hoja ya
kusema uchochezi juu ya habari zinazoandikwa mbona kuna chombo cha
habari kilichowahi kutoa takwimu za kuonyesha idadi ya Wakristo na
Waislamu, tena kwa kukopi takwimu za mtandaoni? Je, huo sio uchochezi?
Mbona haikuwahi kushughulika na chombo hicho au kwa vile inakimiliki?
Kuna methali moja inasema kuwa ukiona
mwenzako ananyolewa wewe tia maji, ni lazima vyombo vya habari
vitafakari kwa kina uonevu huo unaofanywa na serikali dhidi ya tasnia
hiyo. Kama hatutakuwa na umoja na baadhi kuchekelea lile linalowakuta
wengine ni wazi tutakuwa tunajidanganya.
Leo vyombo vya serikali kama vitakuwa
vinachekelea hayo, kuna wakati utafika navyo vinaweza kujikuta muhanga
wa uonevu huu. Ndiyo, kuna mabadiliko yanayoweza kutokea katika taifa,
kuna kuanguka kwa serikali hatua inayoweza kupelekea vyombo hivyo
vikachomwa na mwiba huo huo unaochoma vyombo ambavyo sio vya serikali.
Ndiyo maana nasisitiza kuwa hakuna shangwe katika jambo hilo, ni lazima
tukae kwa umoja na kutafakari wapi tunapohitaji kuelekea.
Kama tupo tayari kuendelea kuonewa na udhalimu huu huku wengine wakiumia, nayo inahitaji tafakari.
Lakini nikumbushe tukio la kuhuzunisha,
la kinyama lililotokea mwaka mmoja uliopita ambapo Jeshi la Polisi
linahusishwa na mauaji ya mwanahabari mwenzetu wakati akiwa kazini.
Unafikiri tukio lile lilistahili kumpata Daudi Mwangosi? La asha.
Linaweza kumkuta yeyote yule aliyeko katika tasnia hii, haijalishi ni wa
chombo cha serikali au cha mtu binafsi.
Ndiyo maana hata katika tukio hilo la
kusikitisha baadhi walitolea wito kwa wanahabari ‘kulisusia’ Jeshi la
Polisi ambalo lilihusishwa na mauaji ya mwandishi huyo. Lakini baadhi ya
wanahabari walipuuzia wito huo ambao ulipaswa kufikisha ujumbe muhimu
kwa jeshi hilo kuhusu haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari.
Ukitafakari kwa kina hakuna hoja ya
msingi unayoweza kuiona katika kuyafungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania, ni utashi binafsi wa wasimamizi wa serikali uliowaongoza na
wala sio madhara ya uchochezi kama unavyozungumzwa katika taarifa hizo.
Kama kweli serikali ina nia thabiti ya
kutaka kuhakikisha inaandikwa kwa mazuri, basi inapaswa pia kusimamia
vyombo vyake vya dola katika kutoa haki. Haiingii akilini hata kidogo
kuwa waumini wamezoea kusali bila kusimamiwa, leo wanawekewa ulinzi na
chombo cha habari kinapokwenda kuandika hivyo, unalalamika na kusema
uchochezi. Hivi unaweza kumtenganisha polisi na kuwa na mbwa anapofanya
ulinzi? Hapana ni serikali kuamua.
Mfukunyuku anaamini kuwa tatizo serikali
haitaki kukubali kuwa imeshindwa katika maeneo mbalimbali. Huwezi
kusema eti waraka wa mishahara iliyotolewa na chombo cha habari ni wa
siri wakati taarifa hiyo ilishawahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete
katika sherehe za wafanyakazi juu ya kuongeza mishahara.
Nilitegemea serikali ilalamikie taarifa
kuwa sio ya kweli, labda imepotoshwa na sio huo waraka kuwa wa siri.
Kabla ya kuanza kushughulikia chombo cha habari wangelazimika kumtafuta
mchawi aliyevujisha huo waraka. Hilo lingekuwa la maana. Lakini kitendo
cha kufungia vyombo vya habari ni kutaka kuwanyima Watanzania fursa ya
kupata habari.
Ni vema serikali ikatambua kuwa kukataa
kusikia ukweli hakuufanyi ukweli huo kuwa uongo. Vyombo vya habari
walivyovifungia vimekuwa na mchango mkubwa kwa serikali, na vimekuwa
vikitoa taarifa za muhimu juu ya yanayoendelea ndani na nje ya nchi hii.
Mfukunyuku anaamini kuwa kitendo cha
kuminya vyombo vya habari na kushindwa kusainiwa kwa sheria ya vyombo
vya habari iliyotungwa na Bunge ni kuendeleza udhalimu wa kutaka masuala
yaliyo na muhimu kushindwa kuripotiwa na hata kutolewa kwa umma wa
Watanzania.
Tena kuna kesi iliyofunguliwa juu ya
kupinga sheria hiyo kutoanza kusikilizwa mahakamani kwa miaka minne sasa
kutokana na kutopangiwa jaji wa kuisikiliza. Hivi leo ukiandika juu ya
jambo hilo utaonekana kuwa mchochezi wakati ni kitu cha kweli cha haki
kushindwa kutendeka?
Tusijidanganye hata kidogo kuwa
tukiminya vyombo vya habari ndiyo madudu yanayofanywa na watu wasio
waaminifu yatashindwa kuandikwa. Hata kama wameamua kuingia hadi katika
mitandao ya kijaami, bado masuala ya wizi wa fedha za nje (EPA),
kutoroshwa kwa wanyama wetu, mabilioni yaliyoibwa kwa Watanzania
yanazidi kutunisha akaunti za mafisadi huko Uswisi, nchi yetu kuwa
uchochoro wa kupitisha na kuingiza dawa za kulevya vitaibuliwa tu.
Nimalizie kwa kusema kuwa juhudi zozote
za kuvinyamazisha vyombo vya habari havitalisadia taifa hili na wala
hazitafanikiwa kwa sababu kama wanachokieleza ni ukweli, hata kama
wakinyamaza wao, basi mawe yatapiga kelele.
Makala hii imeandikwa na Betty Kangonga
Source: Tanzania Daima Jumapili