KUMEIBUKA matapeli wanaotumia makanisa
kuwaibia watu fedha kwa kuwadanganya kuwa fedha zao zitaombewa na kupata
mara tatu zaidi ya kiwango walichonacho, pamoja na zawadi ya madini.
Aidha baadhi ya makanisa likiwemo Kanisa
Katoliki na baadhi ya makanisa ya Pentekoste mkoani Pwani na jijini Dar
es Salaam, yamejikuta yakitumiwa kwa utapeli huo na waliotapeliwa
kuachwa wakilia nje ya milango ya makanisa hayo.
Mkoani Dar es Salaam, gazeti hili
limebaini kuwepo kwa utapeli huo ambapo baadhi ya watu katika maeneo ya
Buguruni walitapeliwa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka
miwili sasa kwa kuelezwa na matapeli hao wanaodaiwa kuwa na dawa za
kuwapumbaza akili, wawape fedha ili wakaziombee.
“Zaidi ya watu 20 walitapeliwa Dar es
Salaam mwaka jana, wanafuatiliwa na matapeli wakitoka ama benki, au
kwenye mitandao ya simu kutoa fedha, wanaingizwa mjini kuwa fedha zao
zitayeyuka ikiwa hawataziombea. “Wanapelekwa mpaka kanisani na
wanarubuniwa kwamba mchungaji ataziombea na mwenye fedha atapokea kutoka
kwa Mungu, mara mbili ya fedha hizo baada ya siku kadhaa, kumbe ndio
katapeliwa hivyo,” alieleza polisi mmoja wa kituo cha Buguruni ambaye
hakutaka jina liandikwe gazetini kwa kuwa si msemaji.
Hivi karibuni, tukio kama hilo
limebainika kuibuka kwa kasi mkoani Pwani, ambako watu takribani 10
wanaelezwa kutapeliwa fedha kati ya Sh 300,000 hadi milioni moja kila
mmoja baada ya kutakiwa na matapeli kuwapatia fedha hizo ili wazipeleke
kanisani kuombewa na baada ya siku moja, watapokea mara tatu na zawadi
ya madini ya dhahabu (jiwe moja).
Inadaiwa makanisa kadhaa yamekumbwa na
hili mkoani humo likiwemo Kanisa Katoliki ambapo katika Parokia ya
Mtakatifu Don Bosco, Kibaha- Tumbi, zaidi ya watu wanne kati ya zaidi ya
10 wanaodaiwa kutapeliwa, walilizwa kupitia kanisa hilo.
Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri
Romwadi Mkandala akihubiri katika Misa ya kumuombea marehemu Sabina
Nandi (92) katika Kijiji cha Boko-Timiza, Kibaha mkoani Pwani wiki moja
iliyopita, alitoa tahadhari kwa waumini na wakazi wa Kibaha kuwa macho
kutokana na kuibuka kwa utapeli huo.
“Tena kabla sijaendelea sana, jamani
nyie watu mnaopenda fedha za bure bure, muwe macho, kuna matapeli
wameibuka hapa Kibaha Tumbi, mtalizwa? Hivi kwa usawa huu nani akupe
fedha za bure? “Kuna watu wanadanganya fedha zinaombewa na mapadri
kanisani kwetu, nasema hakuna kitu kama hicho, watu wamelizwa karibia
10, narudia tena hakuna kanisa wala msikiti utaombea pesa zako
ziongezeke mara tatu kimiujiza, huo ni uvivu na wengi mtatapeliwa
msipokuwa macho,” alisema Padri Mkandala.
Akifafanua alisema hivi karibuni, watu
wawili kila mmoja kwa wakati wake, walikutwa nje ya lango la kanisa hilo
wakilia na kuhamaki baada ya kubaini kuwa wamelizwa kiasi kikubwa cha
fedha na matapeli hao.
Wengine walishawahi kukutwa lakini
hawakuwa tayari kujieleza kutapeliwa. Akielezea wanavyofanya, Padri
Mkandala alisema kwa mujibu wa watu waliowahoji baada ya kuwakuta nje ya
lango la kanisa wakilia, walieleza kuwa matapeli hao wanajipanga
kuanzia katika vibanda vya kutolea fedha vya mitandao ya simu, ama
katika benki na wakishajua kiasi cha fedha walichonacho huwafuatilia na
kuanza kuwatapeli.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani,
Ulrich Matei alipoulizwa kuhusu utapeli huo, alisema hakuna kesi
iliyoripotiwa na kuelezea huenda wahusika wanaogopa kuripoti Polisi
kutokana na mazingira ya kizembe ya kutapeliwa kwao.
“Tumejaribu kufuatilia matukio ya wiki
chache zilizopita hapa kwetu, tumekosa kabisa matukio ya aina hiyo,
huenda wahusika wanadai wameripoti kwetu lakini wanaogopa kuja maana ni
uzembe gani huo wa kutapeliwa namna hiyo katika maisha ya leo, watu
wanapenda fedha zisizo na jasho.