WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, William Lukuvi, ameongoza mamia ya waombolezaji katika maziko ya Grace Mbowe (57), ambaye ni dada wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Akitoa salamu za rambirambi katika maziko hayo yaliyofanyika jana katika kijiji cha Nshara wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lukuvi alisema serikali inaungana na familia ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na dada yake.
Alisema serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Grace, na kueleza ni kipindi kigumu kwa familia na ndugu kutokana na mchango mkubwa wa Grace ndani ya jamii waliokuwa wakiupata.
“Tunatambua hapa duniani ni sehemu ya kupita na tunaishi lakini siku moja tutakufa, hivyo Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) amenituma kutoa pole kwani serikali inaungana na familia ya Mbowe katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao,” alisema.
Grace Mbowe alifariki dunia Septemba 29 kwa ajali ya gari katika eneo la Changa Kabuku, barabara ya Segera-Chalinze, akitokea mkoani Tanga akielekea Dar es Salaam, ambapo gari lake liliacha njia na kupinduka.
-Habari leo