Like Us On Facebook

TISHIO LA AL-SHABAAB BONGO...HATARI NO.1

           SIKU chache baada ya kundi la kigaidi la Al-Shabaab kutekeleza mauaji kwenye jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi, Kenya na kusababisha vifo vya watu 69, baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar walipiga simu Global Publishers na kudai kuwa, baadhi ya maeneo Dar yamekuwa na ulinzi dhaifu kuhusu kupambana na ugaidi.
 Walisema maeneo kadhaa Dar hususan yenye mikusanyiko ya watu, wapo wanaopita na silaha kama bunduki bila kugundulika, jambo ambalo walilitafsiri kama hatari kubwa katika nyakati hizi za vitisho vya kigaidi.
WATAHADHARISHA TISHIO LA AL-SHABAAB
Wakazi hao waliendelea kuweka wazi kuwa ujumbe mzito wa kutishia kuilipua Tanzania unaodaiwa kusambazwa na Al- Shabaab siku za karibuni si wa kuupa kisogo kwani ‘mchelea mwana kulia mwishowe hulia yeye’.


 “Ule ujumbe wa kutishia kuilipua Tanzania si wa kuufumbia macho hata kidogo. Sasa kama Wabongo wenyewe wanaingia sehemu zenye watu wengi na bunduki bila kubainika, hamuoni kama ni hatari namba moja hiyo?
“Mimi juzikati tu hapa nilikwenda Mlimani City kukutana na rafiki yangu, wakati nashuka kwenye gari eneo la maegesho nilishangaa kumwona jamaa mmoja akiweka bunduki vizuri kwenye kiti cha abiria mbele.
“Mnadhani alipitaje pale getini kama si uzembe wa walinzi? Je, kama angekuwa adui anakwenda kuitumia bunduki ile kwenye maduka ya ndani si angefanikiwa?
 “Si Mlimani City tu kwenye ulinzi legelege, kuna Kivuko cha Kigamboni, stendi ya mabasi yaendayo mikoani na Uwanja wa Taifa. Tena pale uwanjani  ni kubaya zaidi kwani ndiyo sehemu inayokusanya watu wengi kwa wakati mmoja nchini Tanzania,” alisema mmoja wa wakazi hao wa Dar.
OFM YA RISASI YAINGIA KAZINI KUCHUNGUZA
Kufuatia taarifa za wananchi hao, makachero wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ ya Global Publishers walianza kutembelea maeneo yaliyotajwa ili  kujihakikishia yanayosemwa na wananchi hao.
UWANJA WA TAIFA
Septemba 29, 2013, saa 10:12 jioni, OFM walizama Uwanja wa Taifa ambapo kulikuwa na mechi kati ya Timu ya Simba na JKT Ruvu, kachero mmoja wa OFM alijaribu kupita getini akiwa ndani ya gari na silaha mbili, bunduki na bastola.

 KACHERO AZAMA NDANI
Kachero huyo alipenya mpaka jukwaani na silaha hizo na kujichanganya na mashabiki zaidi ya 20,000 waliokusanyika kushuhudia pambano hilo kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 waliokaa kwenye siti za watazamaji.
Kachero huyo alipenya kwenye mageti yote bila kukutana na kuzuizi, hali inayotishia hali ya usalama na kutoa tafsiri kwamba, kweli Al-Shabaab wakitaka wanaweza kupenya kirahisi na kutekeleza ugaidi wao eneo hilo.
Wakati kachero huyo akitembea kuelekea kwenye siti, alipishana na polisi mmoja aliyekuwa bize akizungumza na wadau jinsi ya upatikanaji wa tiketi kuliko ulinzi.
 MLIMANI CITY NAKO
Kachero wa OFM alitazama mpira hadi mwisho, alipotoka aliungana na wenzake na kuanza safari ya kwenda Mlimani City ambako ndiko mpiga simu mmoja alisema alimshuhudia mtu ameingia na bunduki.
Kwenye geti la kuingilia upande wa Mashariki, OFM walisimama kwa sekunde kadhaa kwa ajili ya kuchukua kadi, ndani ya gari walikuwa na silaha zilezile za Uwanja wa Taifa, bunduki na bastola.
 Kachero mmoja alishuka na bunduki mkononi, mwingine alichomeka bastola kiunoni wakatembea wakipishana na walinzi kuelekea kwenye Mgahawa wa Samaki-Samaki na Supermarket ya The Game ambako waliendelea kujiachia.

RIPOTI YA OFM
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili maeneo mbalimbali yaliyotajwa umebaini kuwa vyombo vya  usalama vinaendelea kuchukulia tahadhari inayodaiwa ni ya Al-Shabaab kama wimbo wenye mashairi matamu hivyo kukosa mikakati ya kuzidisha upekuzi getini.
Ingekuwa vyema endapo ulinzi wa maeneo hayo ungeimarishwa zaidi ya ilivyo sasa, mtu akaguliwe kwa umakini bila kujali haraka yake pia zana za ukaguzi za kisasa ziwepo na kuachana na utamaduni wa zamani wa kumwangalia mtu akiwa ndani ya gari na kumruhusu apite huku baadhi ya walinzi wakitoa salamu zenye ishara ya kuomba kupewa ‘chochote’.
* Baadhi ya picha juu ni 'makachero wa Risasi' wakiwa na silaha maeneo ya Mlimani City na Uwanja wa Taifa.
-GPL

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari