Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amemtaka Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza kuacha kumshambulia kwenye magazeti, badala yake atumie muda huu kuandaa majibu ya kuwasilisha kwenye kamati kuu kwa hoja zilizoibuliwa na wakulima nchini.
Nape akihutubia mamia ya wananchi wa Mji wa Vwawa wilayani Mbozi
mkoani Mbeya alionyesha kukerwa na tabia ya hivi karibuni ya waziri huyo
kumshambulia kwenye magazeti kwa maneno ya kejeli badala ya kujibu
malalamiko ya wakulima.
“Katibu Mkuu tumezunguka wilaya nyingi sana nchini hakuna mahali
ambako hakuna malalamiko ya wakulima ambao ni 80% ya Watanzania wote.
Sasa tumemtaka waziri aje kwenye kamati kuu kueleza anatatuaje
changamoto hizi, yeye amekazana kila kukicha kunishambulia kwenye
magazeti, alisema na kuongeza:
Nataka kumpa ushauri wa bure mheshimiwa sana waziri, anachofanya
hanishambulii mimi anawashambulia wakulima kwasababu siongei yangu
naongea malalamiko ya wakulima” alisisitiza Nape
“Nimemvumilia sana lakini sasa nimechoka, kila kukicha anatumia
maneno ya kejeli na vijembe, kwa nini hajifunzi busara ya naibu wake
Adam Malima? aliposikia wito wetu akasema yuko tayari kujieleza kwenye
Kamati Kuu kwa kuwa chama ndiyo mwajiri wake, atazingatia uamuzi wa
chama, yeye waziri kila kukicha Nape…Nape…Nape, kumshambulia Nape
hakuondoi kero za wakulima” alisema.
“Nimesikia leo anasema sina busara! Busara ipi anayohoji? Mie
ninayewatetea wakulima wanaolalamika kulazimishwa kutumia mbolea ya
Minjingu inayounguza mazao yao na yeye anayeleta mbolea hiyo na
kulazimisha wakulima watumie nani anatumia busara hapa?”
“Yeye anayepuuza malalamiko ya wakulima kuumizwa na baadhi ya maofisa
ushirika na mimi ninayetaka hatua zichukuliwe dhidi ya maofisa wake
nani anatumia busara?” alisema na kuongeza:
“Mimi ninayemkumbusha kutembelea mkoa alioutangaza kuwa ghala la
taifa la chakula ambao hajautembelea kwa miaka sasa licha ya kuwa waziri
wa chakula na yeye ambaye hajatembelea nani anatumia busara?”
“Mimi ninayemshauri asikilize kilio cha wakulima wa tumbaku, pamba na
korosho badala ya kusikia kilio hicho miaka nenda miaka rudi na yeye
nani anatumia busara?”Source: Mwananchi