Nature amesema muziki wa zamani ulikuwa na mafanikio kwa kuwa wasanii walikuwa wakiimba kwa staili tofauti.
“Huko nyuma tulifanya muziki wenye ladha zinazotofautiana, kila mtu alijitahidi kufanya kazi yenye utofauti. Staili hii ya sasa maarufu ya kubana pua alikuja nayo Mb Doggy na kwa kweli nilifurahi kwani alikuwa amefanya kitu chenye utofauti,” alisema.
“Lakini hali ni tofauti hakuna aliyekuja na wazo lingine, wote bado wapo palepale. Ni vyema tukajifunza ubunifu ili sanaa yetu isonge mbele.”
Alitoa ushauri kwa wasanii wa sasa kuwa wangeacha kuimba nyimbo za mapenzi na badala yake wageukie jamii ili kuweza kutoa elimu katika nyanja mbalimbali.
“Nikipanda jukwaani naimba nyimbo zangu za mwaka 2000 hadi 2012 lakini zote ni kama ndiyo kwanza nimezitoa, ni kwa namna mashabiki wanavyozipenda,” alisema Nature (pichani).
Alipoulizwa kuhusu hilo, Mb Doggy alisema: “Ubunifu wangu ulikuwa mzuri, namshukuru Mungu nilibuni kitu kinachoishi ila si kwamba nimeua Bongo Fleva. Kilichopo ni kwamba vijana wa sasa wapanue mawazo ili waje na kitu bora zaidi, ni kweli kuwa kila mtu sasa anaimba kama mwenzake.”