Katika hali isiyokuwa ya kawaida na kinyama mama mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Amina, Mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam amedaiwa kumuunguza mtoto Hawa Maulid Mbonde.Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa baba wa mtoto huyo anaishi na mwanamke mwingine huku mama mzazi wa mtoto huyo yuko mkoani Mtwara akiwa ameolewa na mwanaume mwingine.
Aidha habari zaidi zinadai kuwa Maulid Mbonde aliachana na mama wa mtoto huyo muda mrefu na kuamua kuishi na mwanamke mwingine.
Habari zinasema hivi karibuni Mbonde alienda mkoani Mtwara akamuomba mtalaka wake ili aweze kuondoka na mtoto huyo kwa lengo la kuja Dar kumuanzishia shule.
“Baada ya kufika huku alimkabidhi mkewe huyo kuwa huyu ni mtoto wake hivyo anahitaji kupewa huduma zote muhimu,” kilisema chanzo.
Inadaiwa kuwa walikubaliana hivyo wakati shughuli za bwana Mbode ni kusafiri kutoka mkoa moja kwenda mwingine kibiashara.
Siku ya tukio hilo inadaiwa kuwa mama wa kambo huyo alichukua maji ya moto huku mtoto huyo akiwa amelala akamwagiwa mwilini na kumsababishia majeraha makubwa.
Imedaiwa kuwa baada ya mama huyo kufanya tukio hilo alitoroka hadi sasa hajulikani alipo kitu ambacho kimewasikitisha upande wa mwanaume.
Mwandishi wetu aliweza kufanya mahojiano na muunguzi mwandamizi katika wodi ya watoto walioungua Cristin Chilambo na kusema yafuatayo.
“Mtoto huyo alifika katika Hospitali ya Muhimbili akitokea Kituo Kidogo cha Afya Kigamboni na alifikishwa hospitalini hapo na baba mzazi Mbonde mwezi Juni 7 mwaka huu.
“Alikuwa na hali mbaya kitu kilicholazimu wataalamu kutafuta kila namna ili kuweza kuokoa maisha yake na jitihada zao zilizaa matunda na ndiyo maana unamuona akiwa katika hali hiyo,” alisema muuguzi huyo.
Kwa upande wa baba mtoto huyo, Mbonde alisema kwa sasa anaangali hali ya afya ya mtoto huyo baada ya kupata nafuu mambo mengine ya kisheria yataendelea.
“Kwa sasa niko shamba lakini mtoto anaendelea vizuri ninamuomba Mungu apone, ukweli utabainika.” alisema baba huyo kwa njia ya simu.
Akizungumza na mwandishi wetu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Englebert Kiondo alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa. “Lakini mtuhumiwa huyo baada ya kuona kuwa amemjeruhi mtoto aliingia mitini na anaendelea kusakwa,” alisema Kamanda Kiondo.