STAA wa Bongo Fleva mwenye mbwembwe kibao, pia anasifika kwa kuwa msafi na anasemekana ndiye mwenye mkwanja wa nguvu Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ anadaiwa yuko kwenye mchakato wa kumnunulia jumba la kifahari mpenzi wake wa ‘nenda rudi’, Wema Sepetu, Amani limeinyaka hii.
KUNA SABABU?
Kwa mujibu wa chanzo, Diamond ameamua kuingia kwenye kujikamua huko kufuatia taarifa kwamba, mmiliki wa nyumba anayoishi Wema kwa sasa (jina lipo), Kijitonyama, Dar es Salaam amemwamuru mlimbwende huyo kuhama kwenye mjengo wake mara baada ya kumaliza mkataba mwezi Juni, mwaka huu. Awali mjengo huo aliutangaza ni wake.
HEBU SIKIA
“Mwenye nyumba anayoishi Wema kwa sasa amekataa mrembo huyo kuendelea kuishi pale, akimaliza mkataba wake Juni, mwaka huu basi, hataki tena.
“Sasa Diamond aliposikia hilo akamwambia Wema isiwe tabu, akamuahidi kumnunulia nyumba ya kifahari yenye thamani ya shilingi milioni mia moja na ishirini na tano.
“Nadhani hiyo nyumba ipo tayari, ndiyo maana amemtajia na bei. Lakini ninavyojua mimi ipo Mwananyamala,” kilisema chanzo.
KUHUSU NYUMBA YA SASA
Kuhusu nyumba ya sasa, ni kweli ‘kifo cha nyani miti yote huteleza’ kwani Wema anatakiwa kutoendelea na mkataba mpya ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama ya Ilala, Dar es Salaam kuamuru anyang’anywe lile gari lake la kifahari aina ya Audi Q7 lenye usajili wa T 973 BUJ na kukabidhiwa mmiliki wake halali, Shadrack Tweve.
Wema alipewa gari hilo na mwanaume anayedaiwa ni mpenzi wake anayejulikana kwa jina la Clement ambaye alilikopa kwa mmiliki huyo lakini alikuwa akikwepa kulipa deni la shilingi milioni 90.
Akizungumza na mwandishi wetu katika mahojiano maalum yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar, mmoja wa ‘kruu’ ya Wema ambaye hakutaka jina lake lionekane gazetini alisema kwa sasa Wema yuko katika kipindi kigumu baada ya kumwagana na kigogo huyo aliyekuwa akidaiwa kumpa jeuri na kufuatia kuamriwa kuhama kwenye nyumba hiyo.
Chanzo chetu kikazidi kumwaga data kuwa mbali na Wema kuachana na Clement, bado mrembo huyo amekuwa katika kipindi kibaya zaidi baada ya kunyang’anywa gari hilo ambalo ndilo alilokuwa akilitumia.
MKATABA WA NYUMBA ULIVYOKUWA
Mpashaji wetu aliendelea kujuza kuwa mmiliki wa nyumba anayoishi Wema ameamua kusitisha mkataba wa kumuongezea Wema muda wa kuendelea kuishi hapo baada ya kusikia madai ya msanii huyo akitamba kwenye magazeti kuwa mjengo huo ni mali yake na aliununua kwa shilingi milioni 400.
“Mkataba wa awali unaisha Juni, mwaka huu, hivyo hataweza kuendelea kuishi hapo lakini pia hana pesa za kuweza kulipa gharama ya nyumba kama ile, kwa sasa hana jeuri tena,” kilisema chanzo hicho.
Kikaongeza: “Unajua mara baada ya Wema kuingia kwenye nyumba ile na magazeti kuandika kwamba ameinunua, mmiliki wake alimfuata Clement kwa sababu ndiye aliyeingia naye mkataba.
“Akamuuliza inakuaje Wema anatangaza nyumba ni yake? Clement akampoza mwenye nyumba kwa kumwambia kwamba, asiwe na wasiwasi, Wema ni staa, mastaa wa Bongo wanapenda kujisifu, yeye adili na yeye aliyeingia naye mkataba.”
AANZA KUSAKA CHUMBA KIMOJA:
Habari zinadai kuwa mtazamo wa Wema (kama nyumba ya kununuliwa na Diamond itachelewa) ni kutafuta chumba kimoja na kupanga ili maisha yaendelee.
MAMA WEMA ASHAURIWA JAMBO:
Wadau hawakuishia hapo, walifika mbali zaidi kwa kumshauri mama mzazi wa staa huyo, Bi. Mariam Sepetu amchukue Wema na kuishi naye nyumbani kwake, Sinza-Mori, Dar ili kuficha aibu hiyo nzito na kubwa ya binti yake.
“Hata kama kuna tofauti baina yao, namshauri mama Wema amchukue mwanaye waishi pamoja, hii ni aibu ya familia kwa jumla,” alisema mdau mmoja kwa sharti la kutotajwa jina lake.
DIAMOND SASA:
Amani lilimsaka Diamond ili kuzungumza kuhusu madai ya kumnunulia Wema nyumba ambapo alisema:
“Mimi sipendi Wema apate tabu, naweza kumgharamia chochote kile ilimradi atulie tu.”
WEMA ATAFUTWA:
Mwandishi wetu alipomtafuta Wema kwa njia ya simu, iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa, hata mwandishi wetu alipomtumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), bado hakujibu.
CLEMENT NAYE:
Katika harakati zetu za kutetea ukweli, mwandishi wetu alimtafuta kigogo huyo kwa ajili ya kupata ukweli halisi ambapo baada ya mwandishi kujitambulisha, Clement alitoa udhuru wa kwenda kikaoni na kutaka apigiwe baada ya dakika tano.
Baada ya dakika 20, mwandishi alimpigia simu Clement lakini kila ilipoita kwa muda aliikata.