
Wiki
ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto ikiwa imeanza
kuadhimishwa duniani Novemba 25 mwaka huu bado vitendo hivyo vimezidi
kushamiri Mkoani Mbeya ambapo mwanafunzi wa darasa la nne shule ya
msingi Aiport Kata ya Iyela jijini Jacline Staniely [9] ameumizwa mkono
wake wa kushoto.
Jacline
akiongea kwa ridhaa ya mama yake amesema alipigwa kwa kutumia ubao na
mwalimu wa shule hiyo Novemba 19 mwaka huu na mwalimu Kanyika kwa kosa
la kuwa na nywele ndefu.
Mwanafunzi
huyo amedai kuwa siku ya tukio alipigwa vibaya na kumsababishia maumivu
makali ambapo siku hiyo mama yake alikuwa safarini Nairobi Kenya hivyo
hakupata matibabu ambapo alilazimika kumwambia mwalimu
jirani[Bibi]ambaye alimpeleka hospitali kutibiwa.

Picha ya X ray ikionesha kidole kilichovunjika :
Hata
hivyo Jackline amesema kuwa kutokana na maumivu makali alilazimika
kufanya mtihani wa Taifa wa darasa la nne bila kupata matibabu ya
kutosha.
Baada
ya kurejea kutoka safari mama yake mzazi aitwae Rehema Adamson
Ndeje[28] mkazi wa Block T jijini Mbeya amesema baada ya maumivu ya
mwanae usiku ilimlazimu kwenda shuleni ili kujua kulikoni,ndipo
alipoonana na mwalimu Kanyika baada ya kukutanishwa na Mwalimu mkuu.
Mama
Jackine amesema hicho ni kipigo cha tatu kukubwa kwa mwanae kupigwa na
mwalimu huyo ambapo alionesha makovu yaliyodaiwa yalitokana na vipigo
vya mwalimu huyo miguuni akidai majeraha hayo yalidumu kwa miezi mitatu.
Hata
hivyo Rehema aliamua kwenda Polisi Mwanjelwa kutoa taarifa za tukio na
kila alipoitwa mwalimu huyo hakutokea ndipo jalada likapelekwa kituo
kikuu cha kati ambapo mwalimu alikamatwa na mhanga kupewa PF 3 kwa ajili
ya matibabu ambapo alipigwa picha na kuonekana moja ya kidole cha kati
cha kushoto kimeathirika kutokana na kupigwa kwa kutumia ubao.

Mzazi
huyo amesema hana nia mbaya na mwalimu Kanyika lakini kitendo cha
kumwadhibu mwanae mara kwa mara ndicho kimemtia shaka hata kuamua kutoa
taarifa Polisi ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwandishi
wa habari hii alipofika shuleni ili kujua mustakabali wa suala hili, mwalimu alimtoa nje akidai yeye ana majukumu mengine .
Mwandishi
alimtafuta mmoja wa wanaharakati wa kijinsia ambaye alikiri kupokea
lalamiko hilo ingawa alijibu kwa mkato kuwa mtoto huyo kaumia kidogo tu
na ni usanii mtoto huyo kufungwa POP na kwamba bado PF3 haijajazwa kitu
hivyo hawezi kuzungumzia lolote.
Kumekuwa
na malamiko mengi katika Dawati hilo kutokana na matukio kutochunguzwa
kwa wakati , hali inayotoa mwanya kwa vitendo hivyo kuibuka mara kwa mara
na wahalifu kutoroka mkono wa sheria .
Kamanda
wa Polisi Mkoani Mbeya ameahidi kulifuatilia suala hilo na ikibainika
mtuhumiwea atafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu