Like Us On Facebook

Jana Rais Kikwete alikutana na viongozi wa vyama vya upinzani na haya ndo MAAZIMIO yaliyofikiwa


            RAIS Jakaya Kikwete jana mchana alikutana na viongozi wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, kujadili maendeleo ya mchakato wa Katiba mpya nchini na kufikia makubaliano.
 
Katika mkutano huo, viongozi hao kwa pamoja, wameazimia vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini.
 
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana jioni mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, ilifafanua kwamba baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, Serikali imeagizwa itafute namna ya kushirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya sheria hiyo.

Katika azimio la pili, wamekubaliana vyama vya siasa nchini, ambao ni wadau muhimu katika mchakato wa Katiba mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano, wa namna ya pamoja ya kusukuma mbele mchakato huo kwa maslahi mapana ya nchi na mustakabali wa Taifa.

“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa vyama hivyo na wadau wengine nchini,” ilieleza taarifa hiyo.

Viongozi
Awali viongozi hao walikutana na Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam katika mazingira ya maelewano na mwafaka, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ndiye msemaji wa viongozi hao.
 
Wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambao kabla ya muungano huo, walikuwa wameungana pamoja kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
 
Mbali na hao waliokuwa katika muungano wao kupinga muswada huo, mkutano huo pia ulihudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula.
 
Mbali na Mangula, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika pia walihudhuria. Wengine ni Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
 
Pia wapo Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Julius Mtatiro na Martin Mng’ongolwa wa NCCR - Mageuzi.

Muswada wasainiwa
Katika hatua nyingine, taarifa ya Ikulu ilieleza “Vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, viwasilishe mapendekezo yao haraka serikalini, ili itafutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo katika marekebisho ya Sheria hiyo.”
 
Taarifa hiyo ya Ikulu ilithibitisha kuwa Muswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, umeshasainiwa na kuwa Sheria kamili na kinachosubiriwa kutokana na maazimio ya mkutano huo, ni maoni ya vyama hivyo, ili irejeshwe bungeni kwa ajili ya marekebisho.
 
Hivi karibuni wanasheria waliunga mkono utaratibu wa Rais kutia saini muswada huo, kwa hoja kwamba umepitia mchakato sahihi na halali wa Kikatiba.
 
Wanasheria hao walimshangaa mwanasheria mwenzao, Lissu (Chadema) kwa ushauri wake alioutangaza kwa umma, kumtaka Rais asisaini muswada huo.
 
Walifafanua kwamba ushauri huo ni wa kisiasa zaidi, usio na tija kwa uongozi unaofuata utaratibu na sheria. 

Wakizungumza na Habari leo, walisema Muswada huo kama ilivyo miswada mingine ya sheria, una nafasi ya kusainiwa na kama kuna marekebisho, unarudishwa bungeni kujadiliwa na kufanyiwa marekebisho.
 
Wakili wa Kujitegemea, John Mapinduzi alisema kuwa Lissu ni mwanasiasa na anachofanya ni kujaribu kupotosha umma.

 “Lazima muswada huo usainiwe ndipo urudishwe bungeni kwa marekebisho, Lissu ni mwanasisa tu anapotosha umma… sasa utarudishwaje bungeni wakati ulishapita?” Alihoji Mapinduzi.
 
Mwanasheria mwingine wa kujitegemea, Jerome Msemwa alisema kusainiwa muswada huo ni njia sahihi na inafanyika mara nyingi na kama kuna marekebisho, yanafanyika baadaye.
 
“Wabunge kama Lissu waliamua kutoka wenyewe bungeni wakati muswada unajadiliwa… hakuna aliyewafukuza, sasa iweje leo watake usisainiwe? haina maana leo hii kumshauri Rais kutosaini. “Ushauri wa Lissu kisheria hauna maana yoyote, hawezi kumshauri Rais leo asisaini wakati anafahamu kuwa hata baada ya kusainiwa, kuna nafasi ya kurudishwa bungeni na kujadiliwa kwa marekebisho yoyote,” alisema Msemwa.
 
Msemwa alisema Rais asiposaini muswada huo na kuurudisha bungeni, maana yake vikao vya wabunge vilivyokaa Dodoma kujadili muswada huo, vilipoteza muda na fedha za wananchi bure.
 
Lissu katika taarifa yake, alisema kama Rais anataka wamuamini, asisaini muswada huo na akiusaini atakuwa ameendeleza mambo ya ki-CCM.
 
Kabla ya mkutano huo wa jana, NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, walisitisha maandamano yaliyokuwa yafanyike, kumshinikiza Rais Kikwete, asisaini Muswada huo, uliopitishwa hivi karibuni na Bunge.
 
Vyama hivyo viliungana kupinga kusainiwa kwa muswada huo, kwa madai kuwa una vipengele vinavyohitaji mabadiliko na umepitishwa kinyume na taratibu.
 
Akizungumzia uamuzi huo, Profesa Lipumba alisema umoja huo ulishasikia na kuitambua nia ya Rais Kikwete aliyoionesha katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, ambapo alibainisha wazi kuwa atakutana na viongozi wa vyama hivyo kuzungumzia suala hilo la muswada wa Katiba.
 
Kutokana na nia hiyo, alisema vyama hivyo havina budi kusitisha kwanza mchakato mzima wa maandamano na mikutano hiyo ya hadhara, hadi mazungumzo na Rais yatakapokamilika na kutoa dira ya kinachoendelea.

Madai yao
Alisema madai ya umoja huo ni kutaka mchakato wa Katiba shirikishi, utakaoheshimu matakwa ya Watanzania wote wa Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata Katiba iliyotengenezwa na wananchi wenyewe.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari