Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ametoboa siri kuelezea jinsi baadhi ya maamuzi yake yalivyokwamishwa na mawaziri wenzake katika awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alitoboa siri hiyo jana wakati akizungumzia mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mkoani Shinyanga kwa lengo la kukabiliana na tatizo la maji mkoani humo.Mradi huo ulitekelezwa na serikali wakati Lowassa akiwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo katika serikali ya Rais Mkapa. Akizungumza wilayani Kahama, Lowassa alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulipingwa na mawaziri wengi katika Baraza la Mawaziri, lakini ni mawaziri wawili tu ambao waliuunga mkono.
Aliwataja mawaziri waliouunga mkono mradi huo kuwa ni Rais Jakaya Kikwete, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na mwingine ni Mohamed Seif Khatibu, ambaye wakati wa uongozi wa Mkapa, aliiongoza wizara za Habari na Mambo ya Ndani.
Lowassa alitoboa siri hiyo alipokuwa akizungumza katika harambee ya uchangiaji wa Shule ya Msingi ya Kanisa la African Inland (AICT) na kusema kuwa Rais Mkapa anastahili sifa kutokana na mafanikio ya mradi huo ambao uliunufaisha Mkoa wa Shinyanga na mikoa ya jirani.
“Niwapeni siri, nilipendekeza waraka wa kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa Rais Mkapa, naye akaniuliza wale wakubwa tutawaweza, nikamwambia tutawaweza, akauleta katika Baraza la Mawaziri, kule mawaziri wote waliupinga kasoro Waziri wa Nje wakati huo, Rais Kikwete na rafiki yangu Mohamed Seif Khatibu waliuafiki,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Mzee Mkapa baada ya kusikiliza mawazo yote akaamua fedha zitolewe.”
Lowassa alitoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja, kumsifu kwa kuwezesha kupeleka maji mkoani humo akisema kuwa wananchi wa Shinyanga wanayaita maji hayo kwa jina la ‘Malowassa’ ikiwa na maana ya maji ya Lowassa.
-NIPASHE