Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Diwani Athumani alisema Agosti 13 majira ya saa 10:30 jioni kijana Doto alitaka kumbaka binti Wayaga Mwinanira (14) ambaye pia ni nduguye aliyekuwa akichunga ng’ombe porini lakini hakufanikiwa.
Kamanda Athumani alisema baada ya wanandugu kupata taarifa hizo mnamo majira ya saa 5:00 usiku walikusanyika nyumbani kwa kijana huyo kwa lengo la kumkamata lakini alipoonekana kuwa mbishi walianza kumshushia kipigo hadi pale mmoja wao alipompiga fimbo kichwani na kusababisha afariki papo hapo.
Alisema kutokana na tukio hilo, wanandugu watano wanashikiliwa na jeshi hilo ambapo aliwataja kuwa ni pamoja na Muondela Jinai (30), Shigela Sodela (33), Gere Mwinanira (39), Moshilo Mwinanira (22) na Vengo Sodela (29) wote wakazi wa kijiji cha Mabadaga.
“Tunaendelea na taratibu mbalimbali za kisheria ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani. Kwa upande wa mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na tayari tumewakabidhi wanandugu kwa ajili ya maziko,” alisema kamanda wa polisi.