Like Us On Facebook

WARIOBA AWATAKA WANASIASA WAACHE KUIJADILI TUME YAKE NA BADALA YAKE WAJADILI RASIMU YA KATIBA KWA MANUFAA YA WATANZANIA


              MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewataka wanasiasa kujielekeza katika kuijadili rasimu ya Katiba iliyotolewa badala ya kuijadili tume na wajumbe wake.
 
Jaji Warioba alisema tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa kuamini kuwa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kwamba ni vema wananchi na wanasiasa wakajadili rasimu ya Katiba iliyotolewa.
 
“Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia tume na watu.
 
“Na siamini kama kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao,” alisema.
 
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo jana wakati akikanusha tuhuma zilizoelekezwa kwa tume yake na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, kwamba tume hiyo imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.

Alisema kuwa siku zote tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa badala ya kuishambulia tume au wajumbe wake.
 
“Moja ya kazi za kisheria za tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote,” alisema.
 
Bulembo alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi akiwa mkoani Tanga ambapo alisema kuwa Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.

Akijibu upotoshaji huo, Jaji Warioba alisema kuwa katika mikutano ya mabaraza ya Katiba ya Wilaya, wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa mabaraza hayo walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na wajumbe wa tume walitoa elimu kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.
 
“Sasa Bulembo anaona kutoa elimu ni dhambi?” aliuliza Warioba ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais.
 
Jaji Warioba alikumbusha kuwa tume yake imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa mbalimbali na kuongeza kuwa pamoja na kauli hizo tume yake inafarijika na kauli za kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.
 
“Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi yaliyoifanya kazi ya tume kuwa ngumu katika mikutano ya mabaraza ya Katiba.

“Matamshi mengine yalilenga tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au wajumbe wa tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema.

-Tanzania daima
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari