Ukosefu wa fedha za kununulia dawa za kulevya, umewafanya
walevi, ‘mateja,’ kubuni njia ya hatari, kwa kunyonya damu yenye kilevi
toka kwa aliyetumia na kujidunga.
‘Mateja’ wamefikia hatua ya kuchangishana fedha na
kununua kete moja ya dawa aina ya heroin yenye ubora, mmoja wao hutumia
na akilewa wengine hupata ulevi huo kwa kumnyonya damu kwa kutumia
sindano ya hospitali na kujidunga.
Reuben (si jina lake halisi) aliyenyong’onyea
mwili mwenye midomo yenye rangi nyeusi anasema aliwahi kubadilishana
damu na watu zaidi ya 20, damu anayoeleza kuwa alikuwa akibadilishana
vijiweni, kwenye kumbi za starehe na maskani bila kuzingatia taratibu
wala athari zake.
“Nimewahi kununua damu kwa watu waliotumia heroin
halisi, pia ‘maskani’ (kijiweni) tulikuwa tukichanga fedha na kununua
heroin halisi kisha mmoja anatumia na baadaye tulichukua damu kwake kwa
njia ya bomba la sindano,” anasema Reuben akiwa kwenye foleni ya
matibabu ya kliniki ya ‘Methadone’ iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Ukishatumia sana ile ya buku baadaye unakuwa
huridhiki sana hata hivyo itakulazimu utumie zaidi ya moja kwa siku,
kwani ile huchakachuliwa sana kwa kuchanganywa na vidonge aina ya
‘Valium’ ambavyo hutumiwa kama dawa za usingizi,” alisema Reuben. Heroin
ambayo huuzwa kwa gharama ya kuanzia sh 1,000 kwa kete hasa ile
‘iliyochakachuliwa’, asilimia kubwa wamekuwa wakishindwa kununua heroin
halisi ambayo huuzwa kwa bei ya juu, hivyo huishia kuomba au kununua
damu kwa aliyetumia aina hiyo ili kupata ulevi.
Akizungumza na gazeti hili, Mtaalamu wa Afya ya
Akili (psychiatric) na Mkuu wa Kliniki ya Matibabu ya Dawa za Kulevya
‘Methadone’ kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Frank Masao, anasema
tatizo hilo wameligundua hivi sasa baada ya kuzungumza na waathirika wa
dawa hizo.
“Baada ya kuzungumza na waathirika hawa tumegundua
kuwa wamekuwa na mazoea ya kubadilishana damu, pindi mmoja anaposhindwa
kununua heroin, wao hawazingatii makundi ya damu wanatoleana tu,
vitendo hivi vimekuwa vikifanywa sana kwa mazoea bila kujali athari za
mbeleni,” alisema Dk Masao.
Hata hivyo, Reuben anasema alianza kubadilishana
damu mwaka 2009, wakati huo walikuwa wakinunua Kinondoni kwa Manyanya,
jijini Dar es Salaam.
“Maskani ambayo nilikuwa nanunua unga ni Kinondoni
kwa Manyanya, pale mpaka mara ya mwisho naachana na dawa za kulevya
mwaka mmoja uliopita, nilikuwa nanunua hapo. Japokuwa nikisafiri
nilikuwa natafuta hukohuko mkoani pia zipo ilimradi upewe ramani na watu
wanaojua soko lilipo,” alisema Reuben.
Amina anayeishi Temeke jijini Dar es Salaam, naye
ni mmoja kati ya waathirika wa zoezi la kubadilishana damu na hakumbuki
idadi kamili ya watu aliokuwa akibadilishana damu japokuwa anasema si
wengi.
“Nilikuwa natumia heroin nyeupe na ile ya brown
miaka 14 iliyopita, wakati huo nilikuwa nafanya shughuli za biashara,
nilikuwa vizuri kifedha lakini leo kama unavyoniona nimechoka,” anaanza
kwa kusema mwanamke huyo aliyejichora ‘tatoo’ nyingi mwilini mwake.
“Nilifika hapa Muhimbili baada ya kuzidiwa na dawa
hizi na uchumi wangu uliyumba, ilifikia hatua nilianza kubadilishana
damu na wengine na hata niliiba na kupora ili tu nipate ‘unga’ kwani
nikienda kuomba kazi walinikatalia na kuniita teja, sikuwa na sehemu ya
kuniongezea kipato. Nawashukuru Asasi ya Blucose ambao walinileta hapa,”
anasema Amina na kuwataka wanawake kutojiingiza katika matumizi ya dawa
za kulevya.
Hata hivyo, Dk Masao amefafanua kuwa matumizi ya dawa za kulevya
humfanya mtu yoyote aliyeambukizwa Virusi vya Ukimwi CD4 zake kushuka
haraka, huku akipoteza uwezo wake kiutendaji na hata akili yake
kuathirika kwa kiwango kikubwa.
Alisema maambukizi ya virusi vya Ukimwi yapo juu
sana kwa waathirika wa dawa za heroin waliofika katika kituo hicho kwa
ajili ya matibabu ya methadone, lakini hata hivyo wapo walioambukizwa
homa ya ini, hao hugundulika baada ya vipimo kwani mwathirika yeyote
lazima afanyiwe vipimo vyote ili kupatiwa matibabu kwa urahisi,
“Asilimia 32 ya wagonjwa wanaotibiwa katika
kliniki hii wana maambukizi ya virusi vya Ukimwi huku asilimia 60 wana
maambukizi ya homa ya ini (hepatitis C) na asilimia 31 wana maambukizi
ya homa ya ini aina ya pili (hepatitis B) huku asilimia 11 wakiwa na
kifua kikuu,” anasema Masao huku akifafanua kuwa watu zaidi ya 25,000
nchini Tanzania wanajidunga dawa aina ya heroin huku 15,000 wakitokea
jijini Dar es Salaam.
Dk Masao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha
Afya ya Akili nchini, anasema Hospitali ya Taifa Muhimbili inahudumia
wagonjwa 640 huku 50 kati yao ni wanawake na kufanya idadi yao kuwa
asilimia saba.
Itaendelea Jumapili ijayo…..
“Kitengo chetu kilianza kutoa huduma hii Februari
2011 na tulianza kupokea wagonjwa wanne kwa siku na ilifikia hatua
tulikuwa tukipokea hata 20 waliohitaji huduma kutoka kwetu na mpaka sasa
tuna wagonjwa 640. Kati ya hawa 18 tuliwaondoa kutokana na matatizo
mbalimbali. Wapo waliokuwa wakifika na silaha mbalimbali na hawa
walikuwa tishio kwa kitengo hiki.”
Dk Masao anasema licha ya kuondolewa katika
kitengo hicho walio wengi wamekuwa wakirudishwa tena; “Hata kama
akifanya vurugu tutamwondoa lakini baadaye lazima tumfuate na kama
akikiri kosa na kuahidi kubadilika tunamrudisha na anaendelea na dozi.
Kila anayetibiwa hapa sharti la kwanza ni lazima makazi yake halisi
yajulikane hivyo inakuwa rahisi kumfuatilia mgonjwa huyu iwapo
atakatisha dozi ili kujua sababu ni nini.”
Akifafanua kuhusu dawa inayotumika kuondoa sumu ya
dawa za kulevya katika mwili wa mwathirika, Dk Masau alisema methadone
humwezesha mgonjwa kutosikia hamu ya kutumia dawa hizo, sambamba na
kumwondolea maumivu mwilini.
“Dawa hii wanayopewa inawasaidia mwili kutokuwa na
maumivu. Maana mtu anaposikia maumivu hapo ndipo anapoanza kuhangaika
kutafuta heroin ili ajidunge. Lakini akipata methadone huwa salama na
hawezi kupata tena hamu ila masharti ya dawa hii ukitumia hupaswi kurudi
tena na kuanza kujidunga,” alisema Dk Masau na kuongeza; “Dawa hii
yenye thamani ya dola 75,000 sawa na Sh124 milioni tumepewa na wafadhili
kutoka Canada ambapo walitoa kiasi cha kilogramu 50 ambazo huweza
kutumika kwa kipindi cha miaka miwili.”
Anafafanua kuwa dozi hiyo hutolewa kila siku
katika hospitali hiyo kwa kiasi cha dozi ya mililita 1.5 kwa kila
mwathirika kila siku huku wengine wakitunzwa wodini kutokana na
kuathirika kwa kiwango kikubwa, hata hivyo aliweka wazi kuwa idadi kubwa
wamekuwa wakishindwa kuhimili gharama za usafiri kila siku.
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuwa na kitengo cha methadone.
“Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa
la Sahara kuanza kutoa matibabu ya methadone, lakini pia tunafundisha
nchi nyingi kutoa huduma hii wakiwemo Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda,
Zambia na nchi nyinginezo ambao hufika hapa Muhimbili kwa ajili ya
kupata utaalamu huu,” alisema Dk Masao.
Alisema utaalamu hasa kuhusu matumizi ya dawa hiyo sambamba na ujuzi wa kutoa matibabu hayo waliupata katika nchi ya Vietnam.
“Vietnam ndipo hasa tulipopata ujuzi huu na huko
tumekuwa tukiwapeleka wataalamu wengi kujifunza. Moja kati ya changamoto
zilizopo katika kitengo hiki ni ukosefu wa watoa huduma, wengi hawapo
radhi kujitolea katika kutoa matibabu kwenye kitengo hiki. Hatuna
wanasaikolojia wa kutosha, manesi na madaktari”
Dk Masao anasema kitengo hicho kimekuwa kikipokea
pia wanandoa ambao wamekuwa wakifika kwa pamoja kwa nia ya kupata huduma
hiyo ili waachane na matumizi ya dawa za kulevya.
“Tunapokea hapa wanandoa wanaohitaji kuacha na
walio wengi huwa waaminifu. Mpaka sasa watu waliopona na kuacha kabisa
tunawatumia katika kuhamasisha wengine kuachana na matumizi ya dawa
hizi.”
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa waathirika wa dawa za kulevya kuwa ni Mbeya, Dodoma, Arusha , Tanga na Morogoro.