RAIS wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein anatazamiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika Paje Mkoa wa Kusini Unguja .
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kamishina ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) Dk Omar Shauri Makame .
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kwamba maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati kunaonekana kuwapo na ongezeko la maambukizi mapya.
Alisema katika mwaka 2012-2013 watu 108 walikutwa na maambukizi mapya na kufanya idadi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi kufikia 6,125 kwa mujibu wa takwimu za watu waliofika katika vituo vya afya kuchunguza afya zao ikiwemo damu.
“Utafiti wa takwimu za ugonjwa wa Ukimwi zinaonesha kwamba yapo maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa kiwango kikubwa ambapo juhudi za makusudi zinahitajika,”alisema.
Kwa mfano alisema Tume ya Ukimwi imeweka mikakati kuyadhibiti makundi hatarishi ikiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya ambapo maambukizi ya kundi hilo yapo kwa asilimia 25.
Mapema Dk Shauri aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi wiki ijayo ambapo ujumbe ni mapambano ya Ukimwi kwa wote yakiwa na lengo la kuwashirikisha watu wenye rika tofauti.
Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa Zanzibar yapo kwa asilimia 14 kwa zaidi ya miaka mitano sasa.