POPOTE utakapotulia na kutazama pambano lolote litakaloonyeshwa moja kwa moja au kwa marudio, kupitia kituo cha Televisheni cha Azam (Azam TV), usiwe na shaka, utaliona pambano maridadi.
Weka soda yako sebuleni kando kisha watazame Jerry Santo na Amri Kiemba wakichuana katikati ya uwanja wowote ule wa soka nchini huku kamera nane za Azam TV zinazorekodi pambano lao zikiwachukua kwa umaridadi.
Kamera nane zamrekodi mchezaji
Katika pambano lolote litakaloonyeshwa na Azam TV kutakuwa na kamera nane uwanjani. Huu ni wastani wa juu wa idadi ya kamera zinazopaswa kuonyesha kwa ufasaha pambano lolote la soka ingawa katika mechi za ligi nyingine au michuano mingine kunakuwa na kamera zaidi za kuonyesha mbwembwe mbalimbali.
Kamera hizi ni ghali zikiwa zimegharimu kiasi cha kuanzia dola 180,000 hadi dola 200,000 kwa kila moja. Ndani ya kila kamera kuna mchanganyiko wa mashine ya Sony huku lensi ya kuvutia matukio kwa ufasaha ikiwa ni ya kampuni ya Cannon. Kamera mbili zitakuwa zinakaa katika kila nyuma ya lango la uwanja. Kamera hizi mbili zina kishikilio kirefu na kuifanya ining’inie katika eneo lote la nyuma ya lango kama tunavyoona katika mechi za Ligi Kuu England na michuano mbalimbali.
Katika pande mbili za uwanja, karibu na benchi la kila timu kutakuwa na kamera mbili ambazo watu wanaorekodi mpira wataweza kukimbia nazo huku na kule kwa ajili ya kutokana matukio yanayoendelea katika upande wa kulia na kushoto kuanzia pale anapokaa mwamuzi wa akiba.
Kamera ya nne ni ile iliyosimama katikati ya uwanja, karibu na mwamuzi wa akiba. Kamera hiyo huwa inasimama ilipo na haisogei. Dhumuni kubwa ni kuzivuta kwa karibu sura za wachezaji au mwamuzi inapohitajika.
Jukwaani kuna kamera kubwa zaidi, pengine kuliko zote. Mtambo huu unarekodi mechi yote kwa juu na ni nzuri kwa mwelekeo mzima wa ‘muvu’ kwa timu zote mbili. Lakini pia kando ya kamera hii kuna kamera nyingine kubwa ambayo nayo inadaka kwa haraka matukio ya ndani ya uwanja.
Pia bado kuna kamera ya saba ya mtu ambaye anazunguka katika kando ya uwanja kwa ajili ya kuchukua mahojiano kabla ya mechi, wakati wa mapumziko na mechi ikiisha. Kamera zote hizi saba zina uwezo wa kurekodi na kuvuta kwa karibu tukio lililo umbali wa mita 400 kutoka zilipo. Hii ni sawa na muunganiko wa viwanja vinne vya mpira!
OB Van ya kisasa zaidi barani Ulaya
Kamera hazina kazi yoyote kama huna OB (Outside Broadcasting)Van ya kisasa. OB Van ni gari linalokamata matangazo uwanjani na kwingineko nje ya studio kutokea katika kamera na kurusha katika setalaiti iliyo hewani. OB Van ya Azam TV ni ya kisasa zaidi ambayo ni zaidi ya OB Van zinazotumiwa na kampuni nyingine za Afrika.
Ikiwa imegharimu kiasi cha Euro 4 milioni, OB Van hiyo ililetwa nchini na Kampuni ya Broadcast Solutions ya Ujerumani chini ya mhandisi wake maarufu, Armando Santos ambaye ameondoka nchini jana Ijumaa baada ya kuendesha mafunzo maalumu ya jinsi ya kuitumia OB Van hiyo.
Santos anakiri kwamba hiyo ni OB Van ya kisasa zaidi barani Ulaya na kampuni yao imekuwa ikipokea oda mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza OB Van ambazo zimekuwa zikitumiwa katika michuano mbalimbali duniani kote.
“Tumekuwa tukisambaza OB Van ambazo zimetumiwa katika kombe la dunia lililopita, Olimpiki, Ligi Kuu Ujerumani, Euro 2012 na michuano mbalimbali duniani, si lazima soka tu. Tunatengeneza OB Van kutegemea na mahitaji ya mteja,” anasema Armando ambaye ameanza kazi hii tangu mwaka 1996.
Ndani ya OB Van hii kuna vyumba vinne vyenye kazi mbalimbali. Ni kama uko ndani ya nyumba yako tu. Kuna chumba cha kupokea picha zote kutoka kamera saba uwanjani ambacho kina runinga zaidi ya 10. Kuna chumba cha mchanganya picha ambacho kina runinga zaidi ya 10, kuna chumba cha mtu wa sauti ambacho kina runinga chache.
Kuna tofauti yoyote na Ulaya?
Nilimuuliza swali hili Santos kama kuna tofauti yoyote ya ziada baina ya kuonyesha mechi Ulaya na itakavyokuwa Azam TV. Santos anakiri kwamba Ulaya kuna kamera nyingi zaidi uwanjani, lakini ambazo hazina kazi kubwa zaidi ya zile saba muhimu.
“Wakati mwingine kunakuwa na kamera nyingi zaidi. Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012 kulikuwa na kamera 68. Lakini achilia mbali zile saba za msingi, hizi nyingine zote zilikuwa za kumrekodi mchezaji mmoja mmoja kwa kila anachofanya uwanjani. Nyingine ni kwa kila kocha. Hazifanyi kazi nyingine.
Kuna Kamera inamrekodi Didier Drogba basi, unamrekodi yeye tu hata kama hana mpira. Zile saba ndizo zinazofanya kazi za msingi. Zipo nyingine kwa ajili ya kurekodi watu maarufu tu walio jukwaani au vituko vya jukwaani.
“Lakini hata hizi saba zilizopo, utagundua kwamba tuna kamera tatu zinazoweza kuibia matukio mbalimbali ya majukwaani na sehemu nyingine.”
Mechi za mikoani
Wakati OB Van moja ikiwa imewasili, OB Van nyingine inatarajiwa kuingia muda wowote katika Bandari ya Dar es Salaam ikitokea Ujerumani. OB Van hii ya kisasa, kama ilivyo ya awali, itakuwa na kazi ya kurekodi mechi za mikoani na itakuwa na kamera nyingine saba za kurekodi mpira mwingine kwa ubora ule ule tu.
Fitina nyingine itakayokatwa ni ile ambayo kila uwanja utakuwa na kamera moja kubwa inayorekodi moja kwa moja mechi nyingine 13 au 12 zitakazokuwa zinaendelea katika viwanja mbalimbali vya Ligi Kuu.
Kamera hizo zitakuwa na kadi maalumu ambayo itakuwa imeunganishwa moja kwa moja na OB Van ambayo itakuwa imebaki Dar es Salaam ikiendelea kuonyesha mechi ya siku. Watu wa kwenye OB Van watakuwa wanaziangalia moja kwa moja mechi nyingine na wanaweza kuchomekea bao au kadi nyekundu iliyoonyeshwa katika uwanja mwingine kama wa Mkwakwani kama Coastal Union imepata bao la kuongoza. Bao hilo litaonekana moja kwa moja katika pambano mfano la Azam na Simba likiwa linaendelea Uwanja wa Taifa au Chamanzi.
Pia, mechi za mikoani zitaanza kurudiwa kuonyesha muda wa usiku kwa ajili ya kukata mzizi wa fitina wa kile ambacho kimeendelea mikoani. Huu ni mwisho wa fitina!
Wazungu wamejaa Chamanzi
Nilibahatika kushuhudia mazoezi ya watu watakaokuwa wanarekodi mechi hizo. Shughuli wanayo. Armando Santos anaondoka nchini akiwa ameacha Wazungu zaidi ya watano kutoka Afrika Kusini ambao wana kazi ya kuwafundisha Watanzania kadhaa ambao wamebahatika kurekodi mechi za Azam TV kutokana na weledi wao.
Mpaka kufikia mwanzoni mwa Oktoba ambapo Azam wataanza kuonyesha mechi hizo, inatazamiwa kwamba kundi hilo litakuwa na weledi wa kutosha wa kuanza safari ndefu ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara kwa walau miaka mitatu ya kuanzia kwa mkataba huo.