Imebainika kwamba sababu ya shambulizi la risasi lililotokea Ilala Bungoni, Dar es Salaam Jumanne iliyopita na kusababisha vifo vya watu watatu, ni wivu wa mapenzi uliopindukia.
Akizungumza
nyumbani kwao Ilala Bungoni jana, mmoja wa majeruhi ambaye ndiye
aliyekuwa kiini cha shambulizi hilo, Newa alisema si kweli kwamba
sababu ya mchumba wake, Gabriel Munisi kuwashambulia na kuwajeruhi kwa
risasi yeye na mama yake mzazi, Ellen Eliezer na kumuua mdogo wake wa
kike, Alpha Newa ni kutokana na kusaliti uchumba wao.
Awali,
ilidaiwa kwamba sababu ya shambulizi hilo ni Christine kumkataa Munisi,
(ambaye pia alijiua baada ya kufanya mauaji hayo) na kuchumbiwa na
rubani wa ndege, marehemu Francis Shumila ambaye pia alifariki katika
tukio hilo... “Kwanza Shumila hakuwa mchumba wangu kama ilivyoelezwa.
Alikuwa shemeji yangu, mume wa dada yangu Caroline Newa. Pia hakuwa
rubani wa ndege, bali nahodha wa meli.”
Alisema
amekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na Munisi katika kipindi
kisichofikia mwaka mmoja lakini sehemu kubwa ya maisha yao ikitawaliwa
na misuguano iliyowafikisha polisi mara kadhaa.
Alisema
katika kipindi cha uhusiano wao marehemu Munisi alikuwa akimpiga,
akimkataza kufanya kazi, kusoma na alikuwa na wivu uliopindukia.
Christine
kuona hivyo, aliamua kufanya mipango ya kwenda kusoma katika Visiwa vya
Cyprus kimyakimya pasi na kumuaga, jambo ambalo alisema lilimkera
mchumba wake huyo na kuweka kisasi.
“Nikiwa
huko, Munisi alitafuta mawasiliano hadi akayapata na tukawasiliana na
siku niliporejea alikuja kunipokea uwanja wa ndege lakini cha ajabu,
alinikataza kwenda nyumbani na badala yake akanipeleka moja kwa moja
hadi Mwanza eneo la Kitangiri,” alisema na kuongeza: “Tukiwa njiani
kuelekea Mwanza, katika maeneo ya Singida, alisimamisha gari akaniambia
nishuke, akatoa bastola na kuniuliza kwa nini niliondoka bila ya
kumuaga. Je, nataka kumuacha?”
Alisema
alimwomba msamaha na kuendelea na safari yao. Anasimulia kwamba baada
ya kufika Mwanza, alimpora simu zake zote na kumfungia ndani kwa zaidi
ya wiki mbili hadi alipopanda kwenye dirisha na kuomba msaada kwa
majirani na kuwapa namba za simu za ndugu zake ili wamsaidie kuwapa
taarifa.
Ndugu
zake walianza mchakato wa kuwasiliana na polisi hatua iliyofanikisha
msichana huyo kurudishwa Dar es Salaam... “Hata hivyo niliondoka na
khanga na fulana tu. Vitu vyote niliviacha huko.”
Baada
ya kurudi Dar es Salaam, anasema Munisi naye aliamua kumfuata lakini
safari hii alifikia katika Hoteli ya MM iliyotenganishwa na ukuta wa
nyumba yao na akawa anafuatilia nyendo za familia hiyo.
“Alikuwa
ananitumia meseji kwamba amemuona dada Caro, mama na Alpha na wakati
mwingine anasema ameniona mimi mpaka nguo tulizovaa, tukaanza kupata na
wasiwasi,” alisema.
Wasiwasi
huo ulitokana na historia ya maisha yao ya Mwanza na pia tishio ambalo
anadai kwamba Munisi aliwahi kulitoa kwamba atahakikisha anaiteketeza
familia yote kuanzia Goba anakoishi mama yake (Ellen), Zanzibar
anakoishi mdogo wake (marehemu Alpha) na hapo Ilala.
Anasema walikwenda polisi lakini walielezwa kwamba hayo ni masuala madogo ya mapenzi na kwamba yatamalizwa kifamilia.
Siku
ya tukio Christine alikuwa akitoka kwenda uwanja wa ndege tayari kwa
safari ya kurudi shuleni Cyprus ndipo Munisi alipotokea na kuanza
kumrushia Shumila risasi na baadaye Alpha kisha mama na yeye kabla ya
kujiua.
Akizungumzia
tukio hilo, Caroline alisema mumewe alitabiri kifo chake kabla kwani
baada ya kusikia vitisho vya Munisi, alimtoa shaka Christine akimwambia
kwamba atamlinda hata ikibidi kupoteza maisha yake, jambo ambalo
lilidhihiri.
Alisema
mama yake amepata nafuu na ameruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili alikokuwa amelazwa na mazishi ya mdogo wake, Alpha ambaye
ameacha mtoto mwenye umri wa miezi minane, yamepangwa kufanyika Jumamosi
Goba, Dar es Salaam.
Alisema mipango ya mazishi ya mumewe inafanywa huku akidokeza kwamba huenda akasafirishwa kwenda Mombasa.
-Mwananchi
-Mwananchi