Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema kumekuwa na changamoto ya uharakishaji wa mashauri ya dawa za kulevya hali inayoifanya Serikali kufikia hatua ya kufikiria kuwa na mahakama maalumu.
Pinda aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana, wakati akiahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge hadi Oktoba 29 mwaka huu.
“Nina imani tukijipanga vizuri inawezekana. Iko hoja kwamba, labda tutafika mahala tufikirie kuwepo na mahakama maalumu ya dawa za kulevya ambayo itakuwa na kazi moja tu ya kusimamia mashauri yanayohusu dawa za kulevya,” alisema.
Alisema pia vita vya dawa za kulevya ni shirikishi kwa kwa mataifa mbalimbali duniani na kwamba jitihada hizo hufanywa kwa mikutano ya pamoja.
Pinda alisema hii itasaidia misako ya pamoja, mafunzo ya pamoja na matumizi ya vifaa mbalimbali kupangwa.
Vilevile, alisema jitihada nyingine ni kuhamasisha kutunga sheria kali zinazofanana ili kutotoa mwanya kwa watuhumiwa kupenya na kufikisha dawa za kulevya kwa watumiaji.
“Ni kweli kwamba, vita vya dawa za kulevya haviwezi kukomeshwa na nchi moja, kwa hiyo mapambano dhidi ya wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya yatafanikiwa tu, kwa nchi zote duniani kuungana kudhibiti biashara hii,” alisema.
Aliwataka wananchi wote kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuwafichua na kutoa taarifa za wote wanaojihusisha na biashara hiyo.
Pinda alisema kati ya mwaka 2010 hadi Julai, 2013, mashauri 368 yanayohusu dawa za kulevya yalipelekwa mahakamani, kati ya hayo, 91 yalimalizika kwa watuhumiwa kufungwa na wengine kutozwa faini.
“Kwa sasa kuna takriban mashauri 245 ambayo bado yako mahakamani. Changamoto inayotukabili katika mahakama zetu na Jeshi la Polisi ni kuharakisha mashauri hayo,” alisema.
Pinda alitumia muda huo pia kueleza kwamba anaiombea Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ijazwe hekima na Mwenyezi Mungu, akisema kazi ya utungaji sheria ni ya wabunge wote.
Alisema hayo kutokana na kitendo cha wabunge hao wa upinzani kususia upitishwaji wa muswada wa Katiba Mpya.
---Mwananchi
---Mwananchi