Mkojo kama huo ambao mwanaume huyu anajisaidia kwa kificho, kinyume cha sheria hadharani ni bidhaa ambayo inaweza kusaidia jamii kwa sasa.
JOHANNESBURG, AFRIKA YA KUSINI. JIULIZE , je, umeenda haja ndogo leo asubuhi au la?
Kama jibu ni ndiyo, basi ujue umemwaga kiasi kikubwa cha nishati ambacho pengine kingeweza kuokoa kiasi cha fedha za kulipia bili ya umeme nyumbani kwako. Pia, mkojo una manufaa zaidi kwako ambayo huenda hukuyajua.
Wanayansi na watafiti nchini Uingereza wamevumbua nguvu za mkojo katika kuzalisha nishati ambayo inaweza kuchaji simu kwa muda wa dakika 25 na pia kumwezesha mteja kutuma ujumbe na kuperuzi intaneti.
Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Watafiti cha Bristol wakishirikiana na wenzao wa Maabara ya Robot wanasema kuwa nishati hiyo ya mkojo ni mapinduzi ambayo yatasaidia katika upungufu wa nishati wakati wowote badala ya kutegemea jua au upepo.
Timu ya watafiti hao iliweka mkojo katika chombo maalumu ambao baada ya muda ulizalisha bakteria.
Bakteria hao baada ya kuwa na njaa huzalisha nguvu za kielektroni na kuwa nishati. Elektroni hizo hudondoshwa katika kontena maalumu kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Mmoja wa wahandisi aliyevumbua nguvu za mkojo, Dk Ioannis Ieropoulo wa Chuo Kikuu cha West of England (UWE), Bristol anasema, mkojo ni bidhaa ambayo haiwezi kutupungukia tofauti na bidhaa nyingine kama maji, upepo au jua.
Wavumbuzi hao wanasema mkojo ni nishati inayopatikana wakati wowote hivyo hatua hiyo inasaidia kuwa na uhakika wa kutopungukiwa na nishati hata kwa watu wa vijijini.
Anaongeza kuwa madhumuni hya uvumbuzi huo ni kupata nishati inayopatikana wakati wowote, rahisi kuiunda na itakayowasaidia watu wengi wa matabaka mbalimbali.
“Tumevumbua na tumehakikisha kuwa inafanya kazi. Kilichobaki sasa ni kuangalia uwezekano wa mkojo kutumika katika matumizi ya nyumbani,” anasema mhandisi
Mpaka sasa betri iliyoundwa kwa nishati ya mkojo huo ina uwezo wa kuchaji simu itakayoweza kudumu kwa dakika 25, kutuma ujumbe na kupiga simu kwa sekunde 20.