Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limepiga marufuku madereva wa pikipiki maarufu kama yeboyebo kubeba maiti.
Jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama barabarani, limewaonya madereva hao kuacha mara moja tabia ya kubeba mizigo isiyostahili kwenye pikipiki zao baada ya kubainika kuwa baadhi yao wamekuwa wakibeba maiti.
Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa polisi Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, Severin Mtaki, alisema kuwa hivi karibuni kumeibuka tabia mbaya ya baadhi ya waendesha pikipiki kubeba mizigo mizito isiyostahili ikiwa ni pamoja na kubeba maiti na kwamba kuna matukio kadhaa yametokea katika Wilaya za Tunduru na Nyasa.
Alisema kuwa matukio hayo ya kusafirisha maiti kwa kutumia pikipiki yamekithiri kwenye wilaya hizo ambapo baadhi ya waendesha pikipiki wamekamatwa kwa kosa hilo.
Mtaki alisema askari wa usalama barabarani wameagizwa kuwakamata waendesha pikipiki watakao kiuka agizo hilo na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Hawa wakifika kwetu Mara Wilaya ya Rorya sijui watasemaje kwani kule maiti husafirishwa kwa baiskeli.