Like Us On Facebook

MAMIA YA WATANZANIA WAPO JELA KWASABABU YA DAWA ZA KULEVYA

Kasi ya kukamatwa kwa Watanzania wakiwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi, imezidi kuchukua sura mpya baada ya kubainika kuwa maelfu ya Watanzania wanatumikia vifungo mbalimbali ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi.
China pekee mpaka sasa ina Watanzania 176 wanaotumikia vifungo katika magereza za nchi hiyo, huku asilimia 99 wakiwa wamekamatwa na dawa za kulevya.
Kutokana na kuwapo ongezeko hilo la wafungwa wa dawa za kulevya, China imekataa ombi la Tanzania la kubadilishana wafungwa, ikieleza hatua hiyo itachochea watu wengine kujiingiza kwenye uuzaji wa dawa za kulevya nchini humo.Hatua hiyo imekuja baada ya nchi hizo mbili kutofautiana katika mfumo wa sheria, ambapo China mtu anayekamatwa
na dawa hizo hunyongwa hadi kufa wakati Tanzania mtu anayekutwa na dawa hizo anahukumiwa kifungo.
Akizungumza na Mwanahabari wetu Jumamosi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema: “Takwimu halisi tulizonazo kutoka China pekee zinaeleza kuwa Watanzania 176 wanatumikia vifungo na asilimia 99 ni kwa tuhuma za dawa za kulevya. Kawaida nchi hiyo adhabu yake ni kifo lakini kesi nyingi bado zipo katika uchunguzi ambao huchukua miaka miwili.”
Hata hivyo alisema kutokana na uhusiano mzuri wa nchi hizi mbili, kuna uwezekano mkubwa kwa Watanzania hao kufungwa kifungo cha maisha pamoja na faini.
Aidha, alisema juhudi za Tanzania kuwasiliana na China kuhusu uwezekano wa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa ziligonga mwamba, baada ya nchi hiyo kukataa ombi hilo kutokana na idadi kubwa ya wafungwa hao kutuhumiwa na dawa za kulevya.
“China imekataa kuwa na mkataba wa kubadilishana wafungwa kwani wanahofu kuwa inaweza ikachochea biashara hivyo. Hivyo kinachofanyika ni kuwatembelea wafungwa hao mara kwa mara na kuhakikisha wanapata haki zao na kuwasaidia mawasiliano wao na ndugu zao wanapotumikia vifungo vyao nchini humo.”
Wakati hayo yakibainika, Jumanne wiki hii Tanzania ilisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Thailand, mkataba ambao utawafanya Watanzania waliofungwa nchini humo kuomba kutumikia vifungo vyao nchini.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaeleza kuwa zaidi ya Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, huku 132 wakikamatwa katika nchi nyinginezo.
Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka katika tume hiyo zinadai kuwa hiyo si takwimu halisi ya Watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi, bali imetokana na nchi hizo kutoa taarifa kuhusu Watanzania hao, kwani bado idadi kubwa ya Watanzania wanakamatwa lakini taarifa zao hazijaweza kuifikia tume.
Akizungumza na Mwanabari wetu jana Kamanda wa Polisi Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema tatizo la dawa za kulevya linazidi kuwa kubwa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wasafirishaji na watumiaji hapa nchini.
Takwimu za watu waliokamatwa ndani ya nchi ambao ni raia wa kigeni na Watanzania zinaonyesha ongezeko kubwa kwa mwaka 2012, ukilinganisha na miaka miwili ya nyuma.
“Mwaka 2010 kitengo kilifanikiwa kukamata watu 496 wakiwa na kilo 191 za Heroin, watu 525 wakiwa na kilo 165 za Cocaine, watu watano wakiwa na kilo tano za dawa aina ya morphine, watu 9539 wakiwa na kilo 279,521 za bangi na watu 1351 wakiwa na kilo 10,318 za mirungi na walifanikiwa kuteketeza ekari 296 za bangi.
“Mwaka 2011 Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya kilikamata watu 40 wakiwa na kilo 265 za Heroine, watu 30 wakiwa na kilo 128 za Cocaine, watu 39 wakiwa na kilo 17,257 za bangi na watu 150 waliokamatwa na kilo 100 za mirungi pamoja na kuteketezwa kwa ekari 18 za bangi.
Nzowa anautaja mwaka 2012 kuwa ongezeko lilipanda mpaka kufikia watu 400 waliokamatwa na kilo 260 za Heroine, watu 138 walikamatwa na kilo 151 za Cocaine na wengine 5548 walikamatwa na kilo 48658 za bangi na wengine 847 walikutwa na mirungi yenye uzito wa kilo 2616.
“Katika watu hawa tuliofanikiwa kuwakamata si kwamba wote wanakutwa na shehena ya dawa hizi, tunaweza kukamata watu 20 wakiwa na gramu 200 tu, lakini tunaweza kukamata watu wachache wakiwa na shehena,” alisema Nzowa.
Anasema Februali, 2011 walimkamata mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Shirena akiwa na shehena ya kilo 176 ya dawa za kulevya ambaye alizipitisha kupitia bandari bubu.
“Bandari bubu hizi walio wengi wanapitisha dawa za kulevya kuingiza nchini kupitia majahazi na mitumbwi na wengi wao wanawatumia wavuvi. mfano tulishawahi kukamata kilo 81 za dawa za kulevya zilizokuwa zikisafirishwa na jahazi. Tulishakamata kilo 211 za dawa za kulevya huko Mchinga, Lindi zilizokuwa zikisafirishwa kwa kutumia njia bubu.”
Alisema mwaka 2011 raia wawili wa nje na Watanzania wawili walikamatwa Mbezi Jogoo wakiwa na kilo 176 za dawa za kulevya wakijiandaa kuzisafirisha, lakini taarifa ndizo zilizosaidia.
Taarifa zingine zilidai kuwa katika magereza za Hong Kong kuna Watanzania 200, ambapo 130 kesi zao zimekwishahukumiwa na wengine 70 kesi bado zinaendelea mahakamani.
Ukubwa wa mtandao ndani na nje ya nchi
Kamanda Nzowa anasema mawakala na matajiri wanaosambaza dawa za kulevya wapo ndani na nje ya nchi na wanashirikiana na kubuni mbinu mpya kila uchao.

“Hawa watu wanawasiliana, kwani Tanzania tunakamata watu wakitoka nje ya nchi wakiingia na dawa za kulevya hapa nchini, lakini hawa wamepita nchi kadhaa bila kugundulika, hivyo Watanzania wanavyokamatwa nje ya nchi si kwamba zinatoka kwa uzembe bali hawa watu wana njia nyingi wanazobuni kila siku,” alisema.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari