NYUMBANI kwa aliyekuwa kigogo wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mbezi-Afrikana, jijini Dar, Amatus Joackim Liyumba kumewaka moto baada ya kigogo huyo kuibuka na askari na kumtoa kwa nguvu mkewe, Aurelia Paul Ngowi na wanae wawili. Tukio hilo lilijiri Agosti 26, mwaka huu ambapo Liyumba alifika eneo hilo akiwa ameongozana na ‘difenda’ mbili na askari wapatao 15 wa Kituo cha Polisi Kawe. Hata hivyo, aligonga mwamba baada ya mwanamke huyo kumpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Englibeth Wambura ambaye aliwaamuru askari hao kuondoka mara moja eneo hilo.
Liyumba hakuishia hapo, na yeye aliondoka, baadaye alirudi akiwa na walinzi 40 wa Kampuni ya Ulinzi ya Kiwango ambao waliitoa familia hiyo kwa nguvu.
Amani lilizungumza na mke wa Liyumba ambaye alisema hakubaliani na uamuzi huo.
“Ukweli sijaridhika na hili haliwezi kwisha hivihivi mpaka haki itendeke, ninajipanga na wakili wangu ili nipate haki yangu,” alisema mwanamke huyo
Zoezi hilo limefanyika baada ya Mahakama ya Kinondoni, Dar hivi karibuni kutupilia mbali pingamizi la mwanamke huyo kumtaka Liyumba ambaye inadaiwa wameachana asiwatoe kwenye nyumba hiyo ambayo pia ina eneo la biashara inayoitwa Amajen Executive Hotel.