Like Us On Facebook

KIKWETE AKABIDHI MAJINA YA WAUZA ‘UNGA’ KWA KAMISHNA....

KAMISHNA wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, amesema baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwakabidhi majina ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kitengo chake kimewafuatilia watuhumiwa na kuwakamata baadhi yao.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamishna Nzowa alisema miongoni mwa waliokamatwa ni wale waliotajwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni, ambapo walipelekwa mahakamani chini ya kiapo maalumu.




Nzowa alitoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua kama kitengo chake kimekwisha kujishughulisha kuyapata majina yaliyokuwa kwa Rais Kikwete na kuyafanyia kazi.

Aliwataja baadhi ya watu waliokamatwa kuanzia mwaka 2007 na kupelekwa mahakamani chini ya kiapo maalumu kuwa ni Ally Hatibu, Ayubu Kiboko na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Shikuba.

“Kiukweli ni wengi wanatajwa, nasi tunafanya kazi na wengine tumewafikisha mahakamani chini ya kiapo maalumu kwa kuwa tunakuwa hatuna ushahidi wa moja kwa moja dhidi yao,” alisema Nzowa.

Aliongeza kuwa mwaka 2011 walifanikiwa kumkamata msambazaji mkubwa wa dawa hizo duniani na kwamba baada ya kumpekua walimkuta akiwa na mifumo (formula) ya kuzuia dawa hizo zisionekane katika mashine.

Alisema vita ya kupambana na dawa za kulevya ni kubwa, inayohitaji watu waaminifu kwa kile alichoeleza kuwa hata mashine za kukaguliwa zinatumiwa na watu ambao wanaweza kuizima pindi wanapotaka kufanya mambo yao.

Nzowa alibainisha kuwa kuanzia mwaka 2007 hadi Julai mwaka huu wameshakamata dawa aina ya heroin zaidi ya kilo 1,000 na cocaine kilo zaidi ya 370.

Alisema dawa hizo zina athari kubwa kwa jamii kwa kile alichoeleza kiasi kinachoweza kumlewesha mtu na kumuathiri ni wastani wa heroin ya gramu 0.11.

Aliongeza kuwa kwa sasa ukamataji umekuwa wa kiwango cha juu nchini, hali inayofanya dawa hizo kuuzwa kwa gharama ya juu tofauti na mwaka 2008.

“Asilimia kubwa ya dawa hizi tunakamata usiku baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na njia kuu ni katika bahari, watu wanatumia bandari bubu kufanikisha mipango haramu ya kuingiza dawa hizi,” alisema Nzowa.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari