MTU
mmoja m kulima na mkazi wa eneo la Kumsenga wilaya ya Kasulu mkoani
Kigoma, aliyefahamika kwa jina la Yusuph Pascal, ameuawa kwa kupigwa na
vitu mbalimbali katika tukio linalodaiwa kuwa ni fumanizi la mapenzi.
Kamanda wa
Polisi Mkoa Kigoma, Fraisser Kashai alisema mjini hapa kwamba mtuhumiwa
huyo wa fumanizi, aliuawa mwanzoni mwa wiki hii.
Alisema baada
ya kifo chake, mume wa mwanamke aliyefumaniwa kwa kushirikiana na watu
wengine, waliuchukua mwili wa marehemu na kuutupa eneo la Mnarani mjini
Kasulu.
Kufuatia tukio
hilo, kamanda huyo alisema watu watano wanashikiliwa na jeshi hilo,
wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo la mauaji ya mkulima huyo.
Kashai
aliwataja watu waliokamatwa kwenye tukio hilo kuwa ni watu watatu wa
familia moja, ambao ni Augustino Adrian, Laurent Adrian na Peter Adrian,
ambao ni wamiliki wa nyumba yalipotokea mauaji.
Aliwataja
wengine waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo kuwa Mihosho Hamza, ambaye
ni mume wa mwanamke aliyefumaniwa akiwa ni mpangaji katika nyumba
yalikotokea mauaji na Raymond Shirima.
Akisimulia
kuhusu tukio, Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai mkoa Kigoma, David
Kisusi alisema awali marehemu akiwa katika nyumba ambayo mwanamke
aliyefumaniwa naye alikuwa akiishi, alivamiwa na watuhumiwa, ambao
walimpiga na vitu vizito na kufariki.
Alisema baada
ya kuona kuwa mtuhumiwa huyo wa fumanizi ameuawa, mume wa mwanamke huyo
na watuhumiwa wengine wanne, waliuchukua mwili wa marehemu na kwenda
kuutupa eneo la Mnarani ili kupoteza ushahidi.
Alisema polisi
walipofika eneo ambalo mwili huo wa marehemu ulikuwa umetupwa, walianza
uchunguzi wao na kubaini kuwa ulitupwa hapo baada ya kuuawa eneo
lingine.
Ndipo
walipofuatilia michirizi ya damu hadi katika nyumba hiyo na kukuta
katika moja ya vyumba hivyo, kuna eneo limemwagiwa mchanga mwingi ili
kuficha damu hiyo ya marehemu.
-Habari Leo.
-Habari Leo.