MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi wilayani Nzega, Tabora, imemhukumu Juma Lufunga (26)
kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa
kaka yake na kumsababishia maumivu makali.
Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Joseph Ngomelo alisema Lufunga (26) ametiwa
hatiani kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka sita na
kumsababishia maumivu makali na hivyo kustahili kifungo cha maisha
gerezani ili adhabu yake iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za
aina hiyo.
Alisema
vitendo vya ulawiti wa watoto wadogo, vimekuwa vikiongezeka kila
kukicha na kusababaisha jamii ishindwe kufanya kazi zingine za maendeleo
kwa hofu juu ya watoto wao kwa kuwa watu wazima wamekuwa ni tatizo hasa
wanaume.
Kabla
ya hukumu hiyo, mtuhumiwa huyo Juma Lufunga akijitetea mbele ya
mahakama hiyo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kutokana na yeye kuwa
ni mwathirika wa virusi vya Ukimwi, hata hivyo mtuhumiwa huyo alipoombwa
vyeti vya uthibitisho hakuweza kuwasilisha mahakamani.
Awali,
Mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi, Melito Ukongoji alidai
mahakamani hapo kuwa Desemba 24 mwaka 2012 majira ya saa 12 jioni katika
kijiji cha Mwanihara, Lufunga alimlawiti mtoto wa kaka yake na
kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri.
Melito alidai taarifa ya daktari ilithibitisha unyama aliofanyiwa mtoto huyo ambaye jina lake linahifadhiwa.