Ni hivi karibuni, Mji wa Geita na maeneo jirani ulikubwa na
taharuki ya aina yake,pale mtoto Shabani Maulid (15) anaedaiwa kwamba
alifariki dunia miaka miaka mitatu iliyopita, alipoonekana akiwa hai
katika Kijiji cha 14 Kambarage, Mtaa wa Mbugani.
Tukio hilo lilizua hofu kwa wakazi wa Mji wa Geita
huku waliowengi wakitaka kujua mtoto huyo aliyekutwa amefariki dunia
baada ya kupotea kwa siku nne mwaka 2011 na mwili wake kuzikwa,
inakuwaje leo hii anaonekana akiwa hai?
Tukio hilo lililotokea Septemba mwaka huu
linashuhudiwa na wazazi wa Shaban, ndugu zake, jamaa na hata majirani wa
eneo hilo ambao pia wanahoji, je aliyezikwa wakati mwili wa mtoto huyo
ulipookotwa ni nani na je mwili wake uko kaburini au la?
Maswali haya na mengine, yalikosa majibu kwani
baada ya kuonekana kwake, Shaban hakuweza kuongea vizuri na alionekana
kutofahamu kabisa Kiswahili, lugha ambayo kabla ya kutoweka kwake
aliifahamu vyema. Wakati huu mtoto huyu anaongea Kiha, japo nayo kwa
tabu.
Hali hiyo iliwalazimisha wazazi wake kushirikiana
na Jeshi la Polisi kumpeleka Haospitali ya Wilaya ya Geita ili apatiwe
matibabu, lakini ni kama hawakuona mtoto wao akipata nafuu hivyo
waliondoka naye na kuamua kumpeleka Kigoma Kambako anapatiwa tiba za
jadi.
“Niliamua nimpeleke kwa waganga wa jadi huku
nyumbani Kigoma na sasa hali inaendelea vizuri kwani anaweza kuongea
japo ni kwa muda mfupi kisha hunyamaza”, alisema baba mzazi wa mtoto
huyo, Maulidi.
Shaban alikuwa wapi?
Shaban hivi sasa anaendelea vizuri na ‘tiba’
anayopata huko Kigoma na aliweza kuzungumza na gazeti hili kwa simu,
huku akieleza kutoweka kwake, pia huko alikokuwa kwa miaka mitatu, huku
akiweka bayana kwamba hivi sasa anawatambua vizuri
wazazi na ndugu zake.
Alisema anakumbuka Januari 1, 2011 aliondoka
nyumbani kwao na kuelekea malishoni kuchunga mbuzi, na wakati akiwa
machungani ghafla lilitokea kundi la watu ambalo lilimzunguka.
Shabani anasema katika kundi hilo alikuwamo
mwanamke ambaye hakumtaja kwa maelezo kwamba anashindwa kutamka jina
lake, ambaye alimshika mkono na kumtaka waondoke eneo hilo.
“Walikuja watu wengi wanaume kwa wanawake, ghaflla
walinizunguka na nikasikia kama kizunguzungu na akili yangu ikawa kama
imezubaa,”alisema Shaban na kuongeza kuwa baada ya watu hao kumzingira
walimwamuru aswage mbuzi zake na kuwarudisha nyumbani.
Alitowekaje?
-Mwananchi
“Niliongozana na watu hao tukiswaga mbuzi hadi nyumbani, lakini
wakati nafika hapo nyumbani hawakuweza kuniona japo mimi nilikuwa naona
kila jambo lilikuwa likiendelea,”anasimulia Shaban na kuongeza:
“Hao watu walionizingira walijibadili sura na
kuonekana kama majirani zetu na mimi pia nilikuwa katikati ya kundi holo
ila wazazi hawakuweza kunitambua.
Alisema kuwa baada ya kukabidhi mbuzi hao, watu
hao waliondoka na yeye alibaki pale nyumbani akiwa na mwanamke
aliyemshika mkono, lakini wakati huo hakuwa akionekana wazi wala
kutambuliwa.
“Tulikaa pale nyumbani kwa nusu saa tangu
tulipofikisha mbuzi na baadaye tuliondoka na huyo mwananke ambaye
alikuwa amenishika mkono, na tukarudi nilikokuwa nachungia na hapo
tuliwakuta wale watu wengine wakiwa wamesimama karibu na dimbwi la
maji,”alisema Shaban.
Alisema baada ya kufika katika dimbwi hilo
walisimama katikati ya maji na baadaye alishtukia akiwa chini ya bahari,
ambako kulikuwa na senta (kituo) kubwa na watu wengi wakiwa wanafanya
shughuli mbalimbali.
“Tulisimama katikati ya dimbwi la maji, gafla
nilistukia niko katikati ya senta kubwa ambayo iko ndani ya maji kama
ziwa,”alisimulia mtoto huyo na kuogeza kuwa eneo hilo kubwa kama mji ama
kijiji ambako watu wanaishi. Hata hivyo kila alipotaka kutaja watu hao
alishindwa kutamka.
“Kunawatu wengi kwenye eneo hilo na mimi
nilistukia tu nikiwa huko na watu wenyewe sikuwajua kwani walikuwa
wageni kwangu,”alisema Shaban.
Hata hivyo alipohojiwa wakati akiwa huko alikuwa
akifanya nini, akila nini na watu wanaoishi huko wanafanya shughuli
gani, alishindwa kuongea na kumkabidhi baba yake simu.
Kwa upande wa baba yake huyo anasema tangu
alipompeleka mwanaye Shaban kwa mganga wa jadi aliyemtaja kwa jina la
Seleman Bundala, aliyeko Kijiji cha Nyankintonto, Kigoma amekuwa akipata
nafuu.
Alisema toka waanze matibabu ya jadi kumekuwa na
mabadiliko makubwa kwani,mtoto huyo alikuwa haongei, lakini kwa sasa
anaongea japo kwa shida na kwamba anaeleza alikokuwa na jinsi
alivyopelekwa.
“Hatoi maelezo mazuri kwani kunawakati anaongea
vizuri na wakati anaonekana kama ulimi unakuwa mzito hasa tunapomuuliza
maswali kwamba ilikuwaje akatoka huko na alikuwa akifanya nini na watu
waliomchukuwa ni akina nani,”alisema Maulidi.
Alitowekaje?
Maulidi alitoweka ghafla Januari 1, 2011. Wazazi wake wanasema
siku hiyo aliondoka nyumbani asubuhi na kupeleka mbuzi malishoni, na
kwamba siku hiyo hakurudi, jambo lililowatia mashaka wazazi wake hivyo
kuamua kutoa taarifa polisi na kwa uongozi wa kijiji.
Taarifa za kupotea mtoto huyo zilienea kijijini
hapo na ndipo walianza juhudi za kumtafuta na baada ya siku nne,
alikutwa amekufa ndani ya kisima cha maji.
“Mtoto wetu aliondoka kwenda kulisha mbuzi siku ya
sikukuu ya mwaka mpya muda wa saa nne asubuhi, hadi inafika saa 12
jioni hakuonekana na badala yake tuliona mbuzi wakiletwa na watoto wa
majirani,”alisema Aziza Ramadhani mama mzazi wa Maulidi.
Aziza ndiye alikuwa wa kwanza kumtambua mtoto wake
katika Mtaa wa Mbugani eneo la Majarubani na wakati huo alikuwa akitoka
kwenye shughuli zake za kibiashara. Anasema alimwona Shaban akikatiza
barabara.
“Nilimuona mwanangu akiwa anakatiza njiani ndipo
nilimuita, Shabani mwanangu ni wewe? Niliposema hivyo alishtuka,
nikaamua kumsogelea huku nikimwita jina lake ndipo alipoitika lakini
hakunitizama usoni,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Baada ya kuthibitisha kwamba ndiye, watu walijaa
na ndipo kwa kushirikiana na majirani tulitoa taarifa polisi, na polisi
wakaja kumchukua na kumpeleka hospitali huku akiwa haongei na tulitumia
ishara kuwasiliana naye”.
-Mwananchi