Like Us On Facebook

Waasi wa M23 waanza kujipanga upya.....Watoto toka Rwanda wapelekwa kuwasaidia waasi hao

 
             WIKI chache baada ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa lililopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO), kulisambaratisha kundi la waasi la M23, kiongozi wa kundi hilo, Bertrand Bisiimwa, ameibuka na kutangaza mkakati mpya wa kujiimarisha ili kurejea katika uwanja wa vita.

Tangazo hilo la Bisiimwa limekuja muda mfupi baada ya Shirika la Habari la Sauti ya Amerika (VOA), kuripoti kuwa masalia ya waasi hao wanajikusanya sambamba na kuandaa vijana wapya watakaopigana sambamba nao.

Taarifa ya VOA iliyotolewa kwanza kabla ya tangazo la Bisiimwa, ilieleza kuwa Rwanda ambayo imekuwa ikidaiwa kuwasaidia waasi wa M23, kwa muda wa miaka 16 imefanikiwa kuwaondoa wanajeshi watoto 3,000 katika jeshi lake. Hata hivyo habari zilizopatikana kutoka Umoja wa Mataifa (UN), zinadai kuwa wapiganaji hao watoto wanaingizwa kwenye vikundi vya waasi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za UN, jitihada za Rwanda kuwaondoa watoto jeshini ni harakati mpya za kuwasaidia waasi wa M23.

Zinamnukuu Mkuu wa Kitengo cha Kumlinda Mtoto wa Umoja wa Mataifa-MONUSCO aliyeko Kinshasa, Dee Brillenburg Wurth, akieleza kuwa Rwanda inaandikisha watoto kwa mfumo maalumu kwa ajili ya kuwapeleka kufanya kazi kwenye kundi la M23 na baadhi yao wana umri wa miaka 11.

Brillenburg amenukuliwa akieleza zaidi kuwa upo ushahidi wa madai hayo, lakini kwa sababu MONUSCO haiwezi kufanya kazi nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wanalazimika kuangalia namna ya kufanya.

Anataja idadi ya watoto 122 waliohojiwa nchini DRC, 37 ni Wanyarwanda ambao walikiri kupatiwa mafunzo ya kijeshi la Jeshi la Rwanda, kuingizwa kwenye vikosi bila kufahamu kuwa walikuwa nchini DRC na wapo pia ambao ni raia wa nchi hiyo.

“Wengi wao walitekwa nyara, kama ilivyo kawaida kwa makundi yoyote yenye silaha, unakwenda kupora au unahitajika kubeba silaha kutoka sehemu moja kwenda nyingine, unachukua watoto kutoka vijijini na huwapi fursa ya kurudi makwao.

“Watoto wengi walianza maisha yao kama watoto wa M23, wakibeba vifaa kutoka mpaka wa Rwanda na Kongo.”

Hata hivyo, tayari Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo, amekwishakanusha taarifa hiyo kwa maelezo kuwa rekodi za mfumo wake wa jeshi zipo wazi, hivyo haiwezi kuvumilia kuona watoto wanaandikishwa katika makundi yoyote yenye silaha.

Wakati Waziri Mushikiwabo akikanusha taarifa hiyo, kiongozi wa waasi wa M23, Bisiimwa, katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na RAI Jumatano, alieleza kuishangaa UN kwa kutoa tamko jeshi la Serikali linaposhambulia wapiganaji wake, lakini imekuwa ikifanya hivyo linaposhambuliwa.

“UN ni wa ajabu sana, inashangaza wanataka sisi tufe, lakini wapiganaji wa jeshi la Serikali wasife, wanakuwa wepesi kutoa vitisho pale tunaposhambulia lakini tukishambuliwa wanaona sawa, sisi hatusaidiwi na mtu, tunachokifanya ni kuipigania nchi yetu, Wakongomani wamechoshwa na Serikali ya kihuni, wanataka kuishi kwenye nchi ya amani kama ile ya Nyerere.

“Hatutaacha kupigana hadi hatua ya mwisho, hatuwezi kuivumilia Serikali hii, waje Uganda tuendelee kuzungumza, sisi tuko tayari kwa mazungumzo kama Serikali itaona ipo haja ya kufanya hivyo, tunataka amani irejee Kongo, kama hawatahitaji kuzungumza tutaendelea kupambana,” alisema Bisiimwa.

Msemaji wa majeshi ya Serikali FARDC, Olivia Amuli, amekaririwa na VOA akieleza kuwa majeshi ya Serikali na yale ya MONUSCO yamekamilisha kazi ya kuwasambaratisha waasi na sasa wananyang’anywa silaha.

Alisema waasi hawatapewa wasaa wa kujipanga upya licha ya kupata taarifa kuwa wanajipanga upya kwa kuwaandaa kwa ajili ya mapigano.

Duru za uchanguzi kutoka uwanja wa vita mjini Goma zinaeleza kuwa eneo hilo linaweza kuendelea kuwa na amani iwapo majeshi ya MONUSCO yataendelea kuwepo huko.

Austere Malivika, mwandishi wa habari aliyejizolea umaarufu wa kuripoti habari za kivita aliyeko mjini Goma, wiki iliyopita alifika nchini na kuzuru ofisi za Mtanzania, ambapo alieleza kuwa eneo la Mashariki mwa Kongo limekuwa katika mapigano ya mara kwa mara licha ya mpango wa amani na kuundwa kwa Serikali ya mpito mwaka 2003.

Alisema kwa sasa hali ni shwari baada ya vikosi vya MONUSCO vinavyoongozwa na wapiganaji wa Tanzania kufanikiwa kuwasambaratisha waasi, lakini hali inaweza kuwa tete iwapo vikosi hivyo vitaondoka.


-Mtanzania
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari