Like Us On Facebook

YULE MWANAMKE GAIDI ALIYEWAONGOZA AL SHABAAB KUIVAMIA KENYA ALIPITIA ARUSHA TANZANIA KUINGIA KENYA



Wakati Serikali ya Kenya imeliomba Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) kumkamata Mwingereza Samantha Lewthwaite (pichani), taarifa zinadai kuwa mwanamke huyo alipitia mpaka wa Namanga, Arusha kwenda Nairobi ambako anahusishwa na tukio la ugaidi.

Lewthwaite, ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Mjane mweupe’ inaaminika anashirikiana na kundi la magaidi la Al-Shabab la Somalia.


Kundi hilo ndilo linaaminika lilihusika na mashambulizi kwenye jengo la Westgate jijini Nairobi, wikiendi iliyopita.


Hata hivyo, taarifa ya Interpol ilisema kuwa alikuwa anatakiwa kujibu mashtaka ya kumiliki mabomu na kupanga njama za ugaidi Desemba 2011.


Interpol haikuhusisha maombi hayo ya Serikali ya Kenya na mashambulizi ya Nairobi.


Pia Lewthwaite inasemekana aliingia nchini humo kwa kutumia mpaka wa Tanzania.


Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini, vinasema mwanamke huyo alitumia pasi ya kusafiri ya nchi hiyo kuingia Kenya kwa kutumia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.


Taarifa hizo zinasema mwanamke huyo alitumia mpaka wa Lunga Lunga na Namanga kati ya Februari na Agosti mwaka 2011 akitumia jina la Webb.


Habari hizo zinaeleza kuwa, awali mwanamke huyo alikuwa anaishi Afrika Kusini ambako aliweza kukopeshwa fedha benki na kuweza kupanga sehemu ya kuishi.


Wakati huohuo, watu wanaodhaniwa kuwa magaidi wamefanya shambulio kwenye Kituo cha Polisi mjini Mandera na kuua askari wawili, kujeruhi watatu kisha kuchoma zaidi ya magari 11 jana asubuhi.


Shambulio hilo ni la pili kufanyika kwenye maeneo mawili tofauti ndani ya saa 24, baada ya lingine lililofanyika kwenye Mji wa Wajir, muda mfupi baada ya taarifa za kudhibitiwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa magaidi walioshambulia jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi.



Shambulio hilo limefanyika wakati kikosi maalumu cha wataalamu wa mabaki ya mabomu wa Kenya na wale wa kimataifa kikianza kufanya upekuzi wa jengo hilo, ili kubaini wahusika halisi wa shambulio hilo na aina ya silaha zilizotumiwa.

Taarifa za awali zilieleza kwamba inadhaniwa waliofanya mashambulizi hayo ni sehemu ya wavamizi hao wanaodaiwa kutoroka, ikiwa ni mkakati wa kuvizubaisha vyombo vya usalama ili kuwawezesha wenzao kutoroka bila vikwazo.

Uvamizi wa jengo la ghorofa nne la Kituo cha Kibiashara cha Westgate uliofanyika Jumamosi iliyopita na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kundi la Al Shabaab na kudumu kwa siku nne ulisababisha vifo vya watu 62 na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Kenya.

Katika shambulio hilo la Kituo cha Polisi Mandera, magari saba kati ya 11 yameharibiwa vibaya kiasi cha kutokutambulika.

Taarifa ya polisi ilieleza kwamba waliofanya shambulio hilo walirusha bomu la roketi (RPG) na kusambaratisha ofisi ya mkuu wa kituo hicho, kisha kutoweka saa 10 alfajiri jana.


Mkuu wa Polisi Eneo la North East aliyemaliza muda wake, Charlton Mureithi alisema watu hao waliwavamia askari polisi waliokuwa wamelala kwenye jengo la utawala.

“Wamesababisha madhara makubwa ikiwemo vifo vya maofisa wetu kisha wakatoroka, lakini tunaamini watakamatwa,” alisema.

Wanadaiwa kutumia muda wao kwenye kituo hicho baada ya kuvamia na kuwafyatulia risasi maofisa hao wa polisi wakiwa karibu.

Walishambulia kwa bomu na kuyalipua kwa kutumia petroli magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye kituo hicho.

Maofisa wa polisi waliojeruhiwa walifikishwa hospitalini mjini Nairobi mchana wa jana kwa ajili ya matibabu zaidi.

Shambulio hilo ni la pili kufanyika ndani ya siku moja baada ya lingine lililofanyika kwenye Mji wa Wajir juzi, ikiwa ni ndani ya saa 24.

Mtu mmoja aliuawa na wengine wanne walijeruhiwa katika mtindo huo wa milipuko ya mabomu iliyofuatiwa na mashambulio ya risasi.

Polisi ilieleza kwamba watu hao wenye silaha walivamia, kushambulia kwa mabomu umati wa watu asubuhi, kisha kuwashambulia kwa risasi na walipokuwa wakitoroka waliwaua watu wawili waliokuwa upande wao na kujeruhi watatu.

Mmoja wa washambuliaji alijeruhiwa na bomu lililolipuka wakati akikimbia, ambapo alikamatwa na kwa sasa anaisaidia polisi.

Mkuu wa Polisi wa Eneo la Wajir, Isaiah Odhiambo alisema kwa sasa wameimarisha ulinzi kwenye eneo hilo.

Wataalamu waanza kazi
Wataalamu wa mabaki ya mabomu wa Kenya na wa nchi za kigeni wameanza kufanya upekuzi kwenye jengo la kibiashara la Westgate, baada ya taarifa za kudhibitiwa kwa wavamizi kwa siku nne.
 
Upekuzi huo umeanza kufanyika huku kukiwa na mkakati wa kimamlaka wa kuhakikisha kwamba mikakati ya taifa hilo katika kukabiliana na ugaidi inapitiwa upya.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya alikaririwa na BBC akisema jana kwamba wataalamu hao wameanza upekuzi huo, huku taifa likiendelea na siku tatu za maombolezo kuanzia juzi.
 
Wataalamu hao wa Kenya wameanza upekuzi huo kwa ushirikiano na Marekani, Uingereza, Ujerumani, Canada na Interpol kwa ajili ya kufuatilia vinasaba (DNA) na alama za vidole ili kubaini wahusika wa tukio hilo.

-Mwananchi
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari