Like Us On Facebook

KITIMOTO CHAUZWA USIKU KWA SIRI


LICHA ya biashara ya nyama ya nguruwe kupigwa marufuku kufuatia mlipuko wa homa ya nguruwe, bado inaendelea kufanywa kwa usiri mkubwa mjini Sumbawanga mkoani hapa. Mapema mwaka huu, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga iliweka chini ya karantini maeneo yote ya tarafa tano kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo mjini Sumbawanga na kupiga marufuku biashara hiyo, maarufu kama kitimoto.
Tarafa zilizowekwa chini ya karantini ni Laela, Mwimbi, Matai, Mpui na Kasanga katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni, umebaini biashara ya nyama hiyo ya nguruwe sasa inafanyika kwa usiri mkubwa katika kitongoji cha Chanji mjini hapa, ambapo imebatizwa majina mapya yakiwemo ‘mchicha, vodafasta na zunguka’.
Imebainika kuwa ni shida kwa mtu ambaye hafahamiki na wauzaji wa nyama hiyo kuhudumiwa, kwa hofu ya kubambwa na maofisa afya, hivyo ili uweze kuhudumiwa bila kutiliwa shaka lazima unapoulizwa na mhudumu nini akuhudumie, lazima utamke majina hayo matatu ya ‘zunguka vodafasta au mchicha’. Vingine huwezi kuhudumiwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa kitimoto walikiri kupata faida kubwa, licha ya kwamba wanaifanya usiku kwa kuogopa kukamatwa na maofisa afya kama wataifanya mchana.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, walikiri kuwa licha ya biashara hiyo kufanyika kwa usiri mkubwa tena usiku, bado nyama hiyo huisha haraka, kwani walaji wake huigombania na kuinunua kwa wingi.
“Kabla ya karantini, nilikuwa nachinja nguruwe mmoja mwenye uzito wa kilo 70, lakini nilikuwa nauza kwa shida sana, baadae ilikuwa inalala, lakini cha ajabu licha ya marufuku iliyowekwa, nachinja nguruwe watatu wenye uzito kati ya kilo 80 na 100 na inaisha mapema tu”, anasema.
Alisema “Tunauza kwa bei ile ile ya awali ya Shilingi 2,500 kwa kilo, lakini bado faida ni kubwa mno kwani inaisha yote, hata kama utakuwa na nyama yenye uzito wa kilo 1,000 au tani moja, lazima itaisha tu, kasi ya walaji kwa sasa ni ya kutisha kuliko ilivyokuwa kabla ya marufuku kuwekwa”.
Baadhi ya walaji wa nyama hiyo ya nguruwe waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi katika kibanda kimoja kinapouzwa, walikiri kuwa licha ya biashara hiyo kufanyika kwa usiri mkubwa, tena usiku, bado wanainunua kwa bei ile ile ya awali.
“Ndugu yangu kumbe kitu chochote kinachofanyika kwa usiri mkubwa ni kitamu, ebu shuhudia hapa jinsi watu wanavyokula hii nyama kwa wingi, wengine wanafungasha na kupeleka nyumbani wakihofia kukamatwa na maofisa wa afya. Hakika hii nyama sasa imepata umaarufu wa kipekee licha ya kuwepo marufuku “, alisema John Aswile, aliyetamba kuwa mlaji maarufu wa nyama hiyo.
Akifafanua, alisema kuanzia saa moja usiku ukifika katika kibanda hicho, utakuta tayari nyama imeshakaangwa na kufungwa katika vifurushi vya kuanzia kilo moja hadi tatu.
Alisema neno ‘zunguka’ linamaanisha kuwa unakula papo hapo, hivyo unazunguka na kukaa mahali palipotayarishwa rasmi. Alisema mteja anapomweleza mhudumu kuwa anataka ‘vodafasta’ moja, anapewa kifurushi cha kilo moja na kuondoka nacho baada ya kulipia.
Akisema anataka ‘mchicha’ anapewa kifurushi cha nyama hiyo, kilichokaangwa pamoja na mchicha. Karantini hiyo ilitangazwa mapema mwaka huu na Daktari wa Mifugo na Mkaguzi wa Mifugo, Dk Seleman Kataga.
Alionya kwamba kuanzia sasa, hakuna ruhusa ya kuondoa kuingiza, kupitisha au kuchinja mifugo katika maeneo yaliyo chini ya karantini. Vilevile alipiga marufuku usafirishaji wa nguruwe kutoka kijiji kimoja hadi kingine ndani na nje ya maeneo hayo.
Alisema “Biashara yoyote ya nguruwe na mazao yake, ikiwemo nyama, mbolea, manyoya, mifupa, ngozi na vyakula vya kusindikwa, imepigwa marufuku iwapo itafanyika bila idhini ya kibali cha maandishi cha daktari mwenye dhamana .“
Katika tarafa hizo zilizokumbwa na mlipuko wa homa hiyo, tayari nguruwe 4,181 wamekufa. Kabla ya ugonjwa huo, kulikuwa na nguruwe 28,630 na sasa wamebaki 24,449.
Ugonjwa huo uliingia wilayani humo kwa mara ya kwanza mwezi Julai 2011 kupitia nguruwe hai, walioingizwa kijijini Chombe Kata ya Kaoze Kata ya Chilulumo Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari