Bondia Francis ‘SMG’ Cheka, amedaiwa kuingia darasani siku moja tu
tangu aliposajiliwa kama mwanafunzi mpya wa Chuo cha St Joseph cha mjini
Morogoro Septemba mwaka jana.
Akizungumza na MWANANCHI, mwalimu wa Cheka aitwaye Mkisi amesema
Cheka ameomba kuendelea na masomo baada ya kutoonekana darasani kwa
miezi kadhaa bila taarifa yoyote, na kubainisha kuwa hawawezi kumruhusu
kuingia muhula wa pili.
Cheka alipewa ufadhili wa masomo chuoni hapo mwaka jana mara baada ya
kutwaa ubingwa wa dunia wa WBF Agosti 30, baada ya kumpiga Phil
Williams wa Marekani katika pambano lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Mkisi amesema kuwa bondia huyo amekosa vipindi kwa muda mrefu hivyo
hawezi kuingia muhula mwingine, kwakuwa atakosa vitu vingi hivyo
anapaswa kujisajili kama mwanafunzi wa muhula mpya utakaoanza Machi 24.
“Cheka aliingia darasani siku moja na ‘kupotea’ hata hivyo hivi
karibuni alikuja na kutuambia anataka kuendelea na shule ingawa hatuwezi
kumuendelezea programu yake ya awali,” alisema Mkisi.
-Mwananchi