Shule
ya Msingi Mtambani iliyoko Kinondoni jijini Dar es Saalam, haina
samani hali inayosababisha wanafunzi kukaa chini, wakati walimu
wanalazimika kutandaza khanga wanazokalia chini ya miti.
wale wasio na nafasi wanakaa chini ya miti”, alisema Mwalimu Mkuu Emmanuel Munisi.
Aliongeza
kuwa tatizo hilo linawalazimisha wengine kutandika khanga chini ya
miti ili kufanya kazi kwa sababu ya ukosefu wa meza za kufanyia kazi
na kwamba mvua inaponyesha wanalazimika kujikusanya pamoja na wanafunzi
madarasani, alisema Munisi.
Shule
ya Mtambani iko taabani wakati serikali ilipata chenji ya rada ya
shilingi bilioni 43 ambayo ilielezwa kuwa pamoja na kununua vitabu
mashuleni pia itawezesha upatikanaji wa madawati.
Serikali
ya Uingereza ilirudisha fedha hizo kuanzia mwaka jana na kwamba jukumu
la kununua vifaa hivyo liliachwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo inasimamia shule za serikali za
msingi na sekondari.
Shule
hiyo ina walimu 41 na wanafunzi 1,830 inakabiliwa na uhaba wa
madawati, viti na meza za walimu kwa mujibu wa Munisi. Aliiambia
NIPASHE Jumamosi kuwa mazingira mabovu ya shule hiyo ni pamoja na
upungufu wa vyoo, ukosefu wa sakafu madarasani badala yake madarasa
yana mahandaki na vumbi kila wakati. Akifafanua, alisema kuwa shule
hiyo ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na wanafunzi 77 na ofisi moja ndongo
kwa ajili ya walimu. Hata hivyo, kwa sasa ina wanafunzi 1,830 wa kike
917, wavulana 913 na walimu 41.
Alisema hakuna maji safi ya kunywa na wanafunzi wengi wanakabiliwa na matatizo ya njaa yanayosababisha kudondoka mara kwa mara.
Alieleza
kuwa wastani wa kuanguka ni kati ya watoto watano na zaidi ambao
hutibiwa kwa kuwekewa drip za kuongeza maji na sukari mwilini.
Madaktari wanasema tatizo ni ukosefu wa chakula na nguvu mwilini kwa
hiyo wanapotundikiwa drip wanapona.
Mwenyekiti
wa Serikali za Mitaa Mtambani, Steven Ngonye, akizungumzia tatizo hilo
alisema litashughulikiwa pamoja na upatikanaji wa maji na ukarabati wa
shule hiyo.
Naye
Diwani wa Kata ya Mtambani Maji Safi Sharifu, alisema serikali
inalitambua tatizo hilo na imetenga bajeti ya Sh. milioni 108 kwa ajili
ya madawati na ukarabati wa vyumba vya madarasa na kwamba hadi sasa
madawati 50 yameshapelekwa shuleni hapo.
Akifafanua
zaidi alisema kuna mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa mawili pamoja
na kufikisha maji safi kazi itakayogharimu Sh. milioni 20.
CHANZO: NIPASHE