Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), imeilipua Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa madai ya kuwa sehemu
ya Mtandao wa Ufisadi serikalini.
Tamisemi
inaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa
Ghasia anayesaidiana na manaibu waziri wawili, Aggrey Mwanry na Majaliwa
Kassim Majaliwa.
Halikadhalika
kamati hiyo ya Bunge imesema, zipo dalili za wazi za kuwapo kwa mtandao
wa kutisha wa kifisadi unawashirikisha baadhi ya watendaji wa
halmashauri nchini, hazina na Tamisemi.
Tuhuma
hizo zilitolewa Bungeni jana na Mwenyekiti wa Laac,Rajab Mbarouk wakati
akiwasilisha taarifa ya hoja za kamati kuhusu hesabu zilizokaguliwa kwa
mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2012.
Alisema
bado kuna ubadhirifu,ufisadi na utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa
matumizi ya fedha za umma kutokana na Tamisemi kutosimamia ama yenyewe
kuhusika moja kwa moja na ufisadi huo.
“Mfano
mwaka 2011/12, Sh1.6 bilioni zilitumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa
katika halmashauri 38 na Sh2.6 bilioni zilihamishwa kutoka akaunti moja
kwenda nyingine bila kurudishwa,”alisema.
Kamati
hiyo imebaini kwamba upo mtindo wa Serikali kutuma kwa halmashauri
kiasi kikubwa cha fedha kuliko kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na
Bunge katika fungu husika wakati wa upitishaji bajeti.
Kamati
hiyo imetolea mfano wa Sh2 bilioni zilizotumwa Halmashauri ya Jiji la
Tanga na Sh500 milioni zilizotumwa katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe
ikiwa ni zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.
“Kitendo
hiki ambacho kinafanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu wa
Hazina,Tamisemi na Halmashauri kinaashiria kuwapo mtandao wa kutisha wa
kifisadi baina ya mamlaka hizo,”alisema.
Kamati
hiyo imeituhumu pia Tamisemi inayoongozwa na Waziri Hawa Ghasia,
kuwahamisha haraka watumishi wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kutoka
hamashauri moja kwenda nyingine.
“Kamati
imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda
watumishi mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini
Tamisemi ni sehemu ya mtandao huu,”imesema.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo alisema kwa makusudi,Tamisemi imekuwa ikieneza saratani
hiyo ya ufisadi kwenye halmashauri nyingi iwezekanavyo na kuitaka
Serikali kuachana na mtindo huo.
Kamati
ya Bunge ya Bajeti, imeishauri Serikali kupunguza matumizi na kuongeza
ukusanyaji mapato ili miradi ya maendeleo igharamiwe kwa asilimia 35 ya
bajeti ya Serikali.
Akiwasilisha
ripoti ya kamati hiyo Bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew
Chenge alisema kwa utaratibu wa sasa hakuna uwiano sawia kati ya
matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo.
Chenge
ambaye pia ni Mbunge wa Bariad Magharibi(CCM) alisema, mwenendo wa deni
la taifa si wa kuridhisha kutokana na kuongezeka kwa mikopo ya masharti
ya kibiashara na malimbikizo ya riba.
-Mwananchi
-Mwananchi