SIKU chache baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kuvuliwa wadhifa wake kwa tuhuma za kushindwa kusimamia wizara yake, kiongozi huyo ametaka apewe moyo wa upendo na kusamehe.
Nchimbi ambaye ni mbunge wa Songea Mjini kwa tiketi ya CCM, alisema
hayo juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook, wakati
akisherehekea kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa.
“Kama Mwenyezi Mungu angeniuliza ni kitu gani anipatie kwa muda huu,
ningemuomba anipatie moyo wa upendo na kusamehe,” aliandika.
Mawaziri wengine waliovuliwa nyadhifa zao pamoja na Nchimbi, ni
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo na Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
“Sasa nina miaka 42, namshukuru Mungu kwa kunibariki na kunisaidia
kwa kipindi cha mwaka mzima, nawashukuru wazazi wangu, kaka, dada na
marafiki zangu, pia ninawashukuru waajiri wangu watu wa Jimbo la Songea
na Watanzania wote.
“Ninaukubali upendo wenu na kuniunga mkono…Kama Mungu ataniuliza leo
kitu gani anipatie jibu langu litakuwa rahisi, nitamwambia Mungu wangu
naomba moyo wa upendo kwa kila mmoja, moyo wa kumsamehe kila mmoja
pasipo kujali nini nitarudishiwa, anipe moyo wa kuwatumikia watu kwa saa
24 kwa siku,” alisema Dk. Nchimbi.
Dk. Nchimbi na wenzake wanne walienguliwa madarakani baada ya Rais
Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao mara baada ya kupewa taarifa za
wabunge kuwashinikiza mawaziri hao wajiuzulu kwa sababu ya
yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kuondolewa kwa mawaziri hao kulitokana na Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kuwasilisha
taarifa ya kamati yake iliyobainisha unyama mkubwa waliotendewa wananchi
katika operesheni hiyo.
Operesheni hiyo ilikuwa ikizihusisha wizara za mawaziri hao
waliong’olewa ambapo inadaiwa watendaji waliokuwa wakiiendesha waliua
watu, kujeruhi na kuharibu mali mbalimbali ikiwemo mifugo.
Matukio mengine yaliyobainika kwenye operesheni hiyo ni wanawake
kubakwa na wengine wakilazimishwa kufanya mapenzi na mama, wakwe au
watoto wao.
source:Tanzania daima
source:Tanzania daima