ILIKUWA ni kama uwanja wa vita na mipasho, ndivyo unavyoweza kusema, baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya Meya wa Halmashauri ya Ilemela, Henry Matata na madiwani wake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Vurugu hizo ziliibuka jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela baada ya Matata kuwataka madiwani watatu wa Chadema kutoka nje ya ukumbi kwa kuwa tayari alikwishawafukuza hivyo si madiwani tena.
Madiwani waliotakiwa kutoka nje ya ukumbi na Kata na zao katika mabano ni Marieta Chenyenge (Ilemela), Abubakar Kapera (Nyamanoro) na Daniel Kahungu (Kirumba).
Hali hiyo ilizua tafrani kwa pande zote mbili kwani walikuwa wakishambuliana kwa maneno makali na ya kashfa huku Meya Matata akitumia nafasi yake kuwaamrisha polisi waliokuwapo ndani ya ukumbi huo kuwatoa nje madiwani hao nguvu.
“Nasema leo hamtakaa ndani ya ukumbi huu na lazima mnijue mimi ndio Meya wenu na posho hamtapata, naomba polisi watoeni nje na mkishindwa nitawaita mabaunsa wangu waingie ndani.
“Wengine hapa mmekuwa mkiombana posho na ndizo zinazowaleta hapa, watu sio madiwani lakini mnang’ang’ania kuja kwenye vikao,”alisema Matata kwa ukali.
Wakati Matata akitoa kauli hizo, madiwani hao nao walikuwa wakimjibu wakidai kuwa hata yeye si diwani wa Chadema, hana kadi na kwamba chama hakimjui na wanashangaa kuona akiendelea kuwa Meya wa Ilemela.
Hata hivyo wakati vijembe hivyo vikiendelea, polisi walishindwa kuwatoa nje madiwani hao na baada ya kutetea haki yao ya kuwamo ndani ya kikao hicho kwa kutumia vifungu kadhaa vya sheria.
Sekeseke lilizidi kupamba moto, pale kitabu cha kujiorodhesha majina kilipofika kwa madiwani hao kwa ajili ya kujiandikisha, jambo ambalo lilimfanya Matata amuagize muhudumu wa Manispaa hiyo kuwanyang’anya.
Hata hivyo muhudumu huyo aliposhindwa kuwanyang’anya kitabu hicho, Matata aliomba msaada kwa polisi ambao nao walikataa hali iliyomfanya ainuke katika kiti chake na kwenda kukichukua kwa nguvu.
Hali ndani ya ukumbi iliendelea kuwa mbaya pia baada ya madiwani hao kunyimwa majoho na taarifa za vikao huku wenzao wa CCM wakipewa huduma zote kitendo ambacho kilionekana kuwakera.
Visa vya Matata havikuishia hapo kwani pia aliamuru meza na viti vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya madiwani kuhamishwa na kuvisogeza mbele karibu na meza kuu isipokuwa vile vilivyokaliwa na madiwani wa Chadema ambavyo viliachwa nyuma.
Katika hali isiyo ya kawaida madiwani hao nao waliamua kuhama walipoachwa na kwenda pale walipokaa madiwani wenzao.
Kitendo hicho kilionekana kumkera Matata na kuamua kutoka nje huku akisema anawafuata makomandoo wake jambo ambalo lilizua hofu kwa baadhi ya wajumbe wengine ambao walikimbilia nje.
Wakati wote wa vurugu hizo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Zuberi Mbyana na Naibu Meya, Sule Debe walikuwa kimya mbele ya meza kuu.
Hata hivyo muda mchache baada ya Matata kutoka nje, Mkurugenzi na Naibu meya nao walitoka nje na kutelekezwa kikao kwa zaidi ya saa moja kabla ya kurejea tena ukumbini.
Baada ya kurudi ukumbini bila makomandoo, kikao kiliendeshwa bila kuwapa nafasi madiwani wa Chadema kuhoji wala kupewa taarifa zozote za vikao licha ya kunyoosha mikono kuhoji hali hiyo.
Kitendo hicho kiliwafanya Madiwani wa Chadema kuwa kama wasikilizaji kwa zaidi ya nusu saa na baadaye kuamua kutoka nje na kwenda Ofisi ya Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia kufanya kikao cha dharura na kutoa tamko.
Wakati kikao cha Chadema kikiendelea, Meya, Mkurugenzi na Naibu Meya waliendelea na kikao hicho kilichokuwa na ajenda ya kupitisha mapendekezo ya kuzigawa tarafa na kata za Wilaya ya Ilemela.
Baada ya kumalizika kikao hicho, Matata alisema alishindwa kuingiza makomandoo wake kutokana na kushauriwa na viongozi wanzake huku akisisitiza kuwa kamwe hawezi kuwaruhusu madiwani hao kuingia kwenye vikao wakati alikwishawafukuza.
Pia aliwalaumu polisi kuzembea kuchukua hatua pale wanapoagizwa huku akimtaka Mkurugenzi kujipanga vema na kuweka ulinzi wa kutosha wakati wa vikao vya aina hiyo.
Tamko la Chadema
Katika taarifa yao waliyoitoa baadaye jana baada ya kikao chao, Madiwani hao wa Chadema walidai kuwa kilichokuwa kikitokea kati yao na Meya ya Halmashauri hiyo ni mkakati wa serikali kutaka kuihujumu Halmashauri ya Ilemela ili isifikie malengo yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiongozi wa Operesheni Kanda ya Ziwa Magharibu, Tungaraza Njugu alisema vurugu zinazotokea Mwanza ni matokeo ya udhaifu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Tamisemi na Rais Jakaya Kikwete.
“Kinachoendelea hapa ni hujuma ambayo inaanzia kwa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Waziri Mkuu, Tamisemi na Rais, mkakati huu wameupanga na kumweka Meya Matata kihuni wakati si diwani.
“Leo hii ni mwaka mzima wananchi wa Ilemela hawana huduma yoyote na barabara zao mbovu, shida hii ni kwa sababu wamekosa wawakilishi badala yake kumeundwa genge ndio linaloendesha Halmashauri.
“Chadema Mkoa wa Mwanza tunaungana kuhakikisha Pinda anaondolewa madarakani kwa sababu ya kushindwa kuziongoza hizi Halmashauri na badala yake analea uchafu” alisema.
Kwa upande wao, madiwani hao walisema wao ni madiwani halali na hata Pinda alitangaza kupitia Bunge lililopita kwamba anawatambua huku wakidai kuwa barua za wao kutambulika zipo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
source:Rai jumatano.