Wabunge Wawili Maarufu wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma
Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wameingia katika vita ya
maneno ambayo chanzo chake ni kauli ya Lema aliyotoa katika kikao cha
wabunge (briefing) kilichofanyika mjini Dodoma Jumanne wiki hii.
Lema akizungumza katika kikao hicho, anadaiwa
kutoa maneno ambayo yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa yalikuwa
yakimlenga Zitto kuhusu hatua yake ya kukataa posho na kumtuhumu kwamba
ana ukwasi ambao unapaswa kuhojiwa.
Mwananchi lilimtafuta Lema likirejea taarifa
iliyotolewa na Zitto akilalamika kwamba Lema alimshambulia katika kikao
hicho cha wabunge wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.
Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha nilichokisema”.
Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa msimamo wa Lema
ulikuwa unapingana na wabunge wengine wa Chadema, ambao waliwahi
kupendekeza kuwa posho zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe, Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika waliwahi
kupendekeza kuwa posho zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, ( posho za vikao ) na
ndo mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011,”
aliongeza Zitto, ambaye anahudhuria mkutano unaozungumzia uendeshaji wa
Serikali kwa uwazi huko London, Uingereza.
Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka sasa ni
makubwa sana ukilinganisha na hali ya wananchi wakati Serikali
ikishindwa kulipa vizuri walimu na wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza kulilia posho,
wakati wananchi wetu hawana maji, hatuwezi kulilia posho. Mbunge
anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza
kuwakilisha watu waendelee,” alisema Zitto.
Lema, hata hivyo, alisema kwamba katika mkutano
huo aliweka bayana kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza kuwa
wabunge wanapaswa kuwa na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu wa
kuwatetea watumishi wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja kupewa
maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni
haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi
wengine,” alisema Lema na kuongeza:
“Kwahiyo nikasisitiza kwamba nawashangaa wale ambao wanakataa
posho ya Sh80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa fedha zote kutokana na
mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu kama Arusha wanalala
kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za Marekani 150 na 600”.
Alisema katika mazingira hayo kunakuwapo maswali
mengi yasiyokuwa na majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo alitakiwa
anapokuwa katika mji wowote nchini aishi katika hoteli yenye thamani
kati ya Sh20,000, 30,000 na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya Sh80,000 halafu
unalala chumba cha Dola 600 hustahili kupata credibility (sifa) stahili,
ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema Lema.
Alisisitiza kwamba wabunge wa Tanzania hawalipwi
ipasavyo na kwamba kudai malipo ya ziada hakuwaondolei wajibu wao wa
kuwatetea watumishi wengine wa umma ambao pia malipo yao ni kidogo.
“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000 au Sh200,000
ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa Sh50,000 basi
maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata
Sh10,000,”alisema
-Mwananchi
-Mwananchi