Nyumba
tano kuchomwa moto, wizi wa mali na watu kupigwa, ni sehemu ya matukio
yaliyotokea katika vurugu za kutisha katika Mji wa Ubaruku wilayani
hapa, Mbeya, juzi jioni.
Vurugu
hizo zimekuja baada ya wakazi wa eneo hilo kukasirishwa na kifo cha
mtoto wa umri miaka 14 anayedaiwa kupigwa na walinzi wa mwekezaji wa
Kampuni ya Mbarali Estates.
Nyumba
zilizochomwa ni za mlinzi mkuu wa kampuni, Atanas Pelela, mgambo wa
kituo kilichomo ndani ya kampuni, Ramadhani Mwamuli na ya Ofisa
Uhusiano wa kampuni, Ignasi Mgao.
Pia
nyumba ya Edison Joseph ambaye hana uhusiano na kampuni, lakini hivi
karibuni alihama kisiasa kutoka Chadema na kujiunga na CCM,jambo ambalo
alisema anahisi kuwa ni kiini.
Nyumba
ya mtu aliyetambuliwa kuwa ni Mafikiri Mwanishuri ilipigwa mawe na
kupasuliwa vioo vya madirisha na yeye mwenyewe kujeruhiwa na sasa
amelazwa katika Hospitali ya Ikonda, wilayani Makete.
Hata hivyo polisi wamefanikiwa kudhibiti vurugu hizo na watu 50 wanashikiliwa.
Tukio
hilo lilitokea juzi saa 12:00 jioni na habari za awali zilisema
vurugu hizo ziliwalenga zaidi walinzi wanaodaiwa kumpiga na hatimaye
kusababisha kifo cha mtoto Lusajo Anosisye (14).
Mtoto
huyo anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali na inasemekana
kitendo hicho kilifanyika Oktoba wakati akikatisha kwenye eneo la
kampuni hiyo.
Kwa
mujibu wa habari hizo baada ya kupigwa mtoto huyo alilazwa katika
Hospitali ya Wilaya ya Mbarali hadi alipofariki dunia juzi jioni. Maziko
yalitarajiwa kufanyika jana.
Diwani wa Kata ya Ubaruku, George Mbillah, alithibitisha tukio hilo huku akibainisha kwamba mtoto alipigwa Oktoba 29 mwaka huu
Mbillah
alisema taarifa za awali zilisema mtoto huyo alipigwa baada ya kupita
kwenye njia inayokatisha eneo la shamba wakati akipita kwenda kukata
matete porini .
Inadaiwa
baada ya kipigo hicho, mtoto huyo alichukuliwa na mkurugenzi wa shamba
hilo na kumpeleka kituo cha polisi na kudaiwa mwizi .Kwa mujibu wa
habari hizo, polisi walimpeleka mahabusu katika Gereza la Rujewa.
Diwani
huyo alisema mtoto huyo aliwekewa dhamana,lakini alipotoka aliendelea
kuumwa na baadaye kupelekwa katika Hospitali ya Rujewa ambako alifariki
juzi.
Baada ya habari kuhusu kifo cha mtoto huyo, wananchi walitaharuki na kuamua kuchoma moto nyumba.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwan Athuman, alisema watu 50 wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.
-Mwananchi
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.