Shilole akijiachia stejini na shabiki.
Katika Bongo Fleva na Filamu, fani zinazokimbiliwa zaidi na vijana,
lipo kundi kubwa la watu wanaotoka kimaisha kupitia huko. Na mmoja wa
vijana wenye vipaji, ni Zuwena Mohamed, ambaye mashabiki wa muziki
wanamtambua kama Shilole.Niwe mkweli, simfahamu msichana huyu kwa maana ya kuwahi kufanya naye kazi, ila nimewahi kusikia kazi zake hasa wimbo wake huu unaotamba sasa, Nakomaa na Jiji.
Pamoja na kwamba bado ni msanii mchanga, lakini ameonyesha kuwa anaweza ubunifu. Wengi wanapenda kuimba, lakini waimbe vipi ndiyo huwa tatizo. Ni kama Snura alivyojishauri na kuamua kuipa kisogo fani ya uigizaji na kujikita kwenye mduara.
Lakini ndani ya fani, Shilole ni aina ya binti anayewakilisha mastaa uchwara wa kike Bongo, wasiojitambua na bahati mbaya, hatambui hata mahitaji ya wateja wake.
Nimewahi kuona mara kadhaa akiandikwa magazetini kuhusu mambo yake mengi yanayokera, hasa aina ya uvaaji. Moja ya jambo lililonitatiza, ni jinsi wakati mwingine anavyovaa blauzi zake tata, zinazoruhusu matiti yake karibu yote kuwa nje!
Lakini nimejikuta nikisita kukaa kimya baada ya kukutana na kauli yake katika moja ya magazeti ya kila siku nchini, akidai kwamba anavaa vile ambavyo watu wamekuwa wakimlalamikia, kwa sababu mashabiki wake ndiyo wanapenda!
Yaani anavyovaa nguo za ajabu ajabu, yaani zenye kuonyesha sehemu kubwa ya mwili wake hadharani, ndivyo ambavyo watu wanaofurika katika majukwaa anayoimba wanavyopenda.
Ni kweli kwamba katika biashara, ni jambo la msingi sana kutazama nini mahitaji ya wateja. Muziki ni biashara na mashabiki ndiyo wateja wenyewe. Sitaki kuamini kama wale watu wanaojitokeza katika matamasha ambayo Shilole hualikwa kutumbuiza wanafurahishwa nayo.
Kwanza ni jambo la msingi kumfahamisha Shilole kwamba hana mashabiki. Nasema hivi kwa sababu kama leo hii mtu atajitokeza na kuandaa shoo ya mtu mmoja tu, ambaye ni yeye, sidhani kama atafanikiwa. Na katika hili, kuna watu wachache sana wanaweza kujaza watu katika nchi hii, wakiongozwa na Nasib Abdul ‘Diamond’.
Shilole anaalikwa katika matamasha kwa ajili ya kuchanganya ladha tu na wala asije akaona watu wanavyopiga kelele anapokuwa jukwaani basi wanashangilia mavazi yake. Huwezi jua, huenda huwa wanamzomea!
Kuvaa ovyo hakuwezi kuwafanya watu waupende muziki wako. Sijawahi kumuona msanii wa kike mvaa ovyo aliyefanikiwa kuuza sana nakala zake katika Tanzania tokea nianze kufuatilia Bongo Fleva. Sana naona wanashindwa tu, wakiongozwa na Ray C!
Lakini kuna wasanii wengi tu wa kike waliofanya vizuri na kujilundikia mashabiki, lakini bado wanavaa mavazi ya heshima jukwaani, kwenye video zao na hata wanapokuwa kwenye matukio ya kijamii. Hapa upo mfano wa Lady Jay Dee kwani ndiye msanii wa kike mwenye mafanikio zaidi lakini anayejiheshimu.
Kwangu, kuvaa mavazi yenye kuonyesha sehemu kubwa ya mwili ni kutojiamini. Anataka watu wavutike kwa kuangalia mwili badala ya kazi. Ndiyo hawa hawa waliojazana katika Muvi zetu, wanavaa nusu uchi kuwachota watu akili ili concentration yao iwe kwenye miili yao badala ya kazi zao!
Tubadilike. Nimesema mara kwa mara, ukishakuwa staa, unapaswa kuwa mfano ulio bora!