JESHI la polisi Mkoani Ruvuma
linawashikilia wanakijiji zaidi ya kumi na tano (15) wakiwemo
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha
Ntunduwalo, Afisa mtendaji wa kijiji hicho na Afisa Mtendaji wa Kata
ya Rwanda kufuatia wanakijiji cha Ntunduwalo kuzuia magari
yanayokwenda na kutoka yakiwa yamesheheni Mkaa ya Mawe toka kwenye
Mgodi wa Mngaka wilayani Mbinga ambako polisi wamelazimika kutumia
mabomu ya machozi kuwatawanya wakati wakizuia magari yaliyobeba makaa
ya mawe mpaka walipwe fedha za fidia wanazodai.
Habari zilizopatikana jana mchana
Mjini Songea ambazo zimezibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa
Ruvuma Deudedit Nsimeki zimesema kuwa tukio hilo lilianza kutokea
juzi majira ya saa za asubuhi ambako wananchi wa kijiji cha
Ntunduwalo walijipanga na kufunga barabara inayokwenda kwenye mgodi wa
makaa ya mawe uliopo karibu na kijiji hicho.
Alisema wanakijiji hao walikuwa na
lengo la kuishinikiza serikali ili iwalipe nyongeza ya fidia ambayo
wanadai kuwa hapo awali walipunjwa wakati wanafanyiwa tasmini ya mali
zao zilizokuwepo ndani ya maeneo yaliyochukuliwa na mgodi huo kwamba
serikali ilitumia sheria ya zamani badara ya sheria iliyopo hivi
sasa ambayo inaonesha kuwa ni kubwa.
Alifafanua kuwa kundi kubwa la
wananchi wakiwemo watoto na akina mama waliokuwa wamekaa mbele
lililojipanga ni lile lililolipwa mwanzo kwa kutumia sheria ya
uthamini ya zamani ambapo wanadai kuwa wamekuwa wakiahidiwa mara kwa
mara na serikali kuwa watalipwa kiasi cha fedha cha fidia
kilichobaki.
Alieleza zaidi kuwa kutokana na hali
hiyo wanakijiji hao waliamua kuchukua uwamuzi wa kuzuia shughuli za
magari yanayobeba makaa ya mawe yasiingie kuchukua makaa ya mawe
iwala kutoka kwenye eneo hilo.
Alibainisha zaidi kuwa kufuatia kuwepo
kwa vurugu hiyo iliyosababisha shughuli za mgodi kusimama polisi
baada ya kupewa taarifa hiyo walikwenda kwenye kijiji hicho wakiwa
wameongozana na katibu tawaa wa wilaya ya Mbinga Idd Mponda ili
kujaribu kuongea na wananchi, kuwasii waondoe kizuizi hicho ili
magari yaendelee na kazi ya kusomba makaa yam awe lakini wananchi
walikataa na walimueleza katibu tawala huyo kuwa hawamuitaji kumuona
yeye pamoja na watu wengine wala Mkuu wa wilaya hiyo kuwasikiliza
wanachotaka walipwe fedha zao wanazodai na si vinginevyo.
Aliongeza kusema kuwa mvutano huo wa
mazungumzo kati ya katibu tawala wa wilaya hiyo Mponda na wanakijiji
yalidumu kwa muda mrefu hadi juzi majira ya saa tatu usiku polisi
waliamua kulilinda eneo hilo na baadaye walifanikiwa kuwakamata watu
watano ambao wanadaiwa kuwa ndio waliokuwa viongozi wa vurugu
hizo.
Amewataja baadhi ya wanashikiliwa kuwa
ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ntunduwalo John Nyimbo
(36), Matrida Nchimbi ( 49) ambaye ni Afisa mtendaji wa kata ya
Rwanda, Joachim Ngaponda ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho,
mwenyekiti wa kamati ya miradi ya kijiji hicho Garusi Komba (49) na
John Joachim Mahai (45) mkazi wa kijiji cha Malindindo tarafa ya
Mbuji wote wanaendelea kuhojiwa na Polisi.
Aidha, Kamanda Nsimeki alisema kuwa
pamoja na polisi kuwashikiria wanakijiji hao jana majira ya asubuhi
vurugu zilirejea tena ambapo polisi walilazimika kutumia mabomu
ya machozi kuwatawanya wanakijiji hao ambao waliendelea kuyazuia
magari yaliyokuwa yamebeba makaa ya mawe huku wananchi wakijitahidi
kuyazuia yasipite.
Hata hivyo jitihada za songeayetu
kumpata mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Mbinga
ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga ziligonga mwamba
baada ya kupigiwa simu kwa zaidi ya mara tatu ambayo haikuweza
kupokelewa na baadaye alipopigiwa simu mara ya nne ilipokelewa na
mtu mwingine ambaye alidai kuwa DC yupo kwenye kikao hivyo hana nafasi
ya kuongea muda huo.