TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Idara ya Habari – MAELEZO, inapenda
kuufahamisha umma wa Watanzania kwamba Mheshiwa Dkt. Fenella Mukangara,
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo amepokea maombi kutoka
kwa wamiliki wa Magazeti ya Mwananchi na Mtanzania wakiomba kupunguziwa
adhabu au kusamehewa adhabu wanazozitumikia kuanzia 27 Septemba, 2013.
Wakati Mheshiwa Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo anatafakari maombi hayo, amesikitishwa
kuona kwamba magazeti haya mawili yamekiuka masharti ya adhabu
walizopewa.
Wamiliki wa Gazeti la Mtanzania baada
ya kufungiwa wameamua kuligeuza gazeti la kila wiki la RAI kuwa la kila
siku bila ya kibali cha Msajili wa Magazeti. Kwa mujibu wa ratiba
,gazeti la RAI linapaswa kutoka kila siku ya Alhamisi.
Wamiliki wa gazeti la Mwananchi nao wameendelea kuchapisha gazeti hilo katika mtandao kinyume na agizo la kufungiwa.
Serikali inawataka wamiliki wa vyombo
vya habari nchini kuwa na utamaduni wa kutii sheria za vyombo vya habari
zinazotumika wakati huu. Hivyo serikali kwa mara nyingine tena
inawataka wamiliki wa Gazeti la MTANZANIA, kuzingatia ratiba yao ya
kutoa gazeti lao kila siku ya ALHAMISI.
Aidha, serikali inawataka wamiliki wa
Gazeti la Mwananchi kuacha mara moja kuchapisha gazeti lao katika
mtandao kama amri ya kufungiwa ilivyoanisha.
Imetolewa na,
Idara ya Habari – MAELEZO
10 Oktoba, 2013Idara ya Habari – MAELEZO