Jeshi la Polisi mkoani Geita,limefanikiwa kuwakamata watu wawili
wakiwa na kadi 243 za watu mbalimbali wilayani Chato, zinazotumika kutolea
fedha kwenye ATM za Benki ya NMB kinyume cha sheria.
Kamanda wa
polisi mkoani Geita, Leonard Paulo,aliwaambia waandishi wa habari ofisini
kwake,kuwa tukio hilo
lilitokea juzi saa 7, usiku katika Kijiji cha Kitela wilayani Chato.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwani Gidion Matiku
(22) na Seleman Hassan(30) mkazi wa Chato wote wakiwa wafanyabiashara wa duka
la nafaka pamoja na vifaa vya ujenzi.
“Tunawashikilia watu
hawa tukiendelea kufanya uchunguzi zaidi kwa nini wanamiliki hizi kadi zote za
ATM zilizotolewa na Benki ya NMB wanazifanyia nini kwa sababu zina majina ya
wateja mbalimbali, ambao ndio wamiliki halali wanaotambuliwa na benki hii na si
wao,” alisema Kamanda huyo.
Alisema, kuwa kitendo hicho cha kumiliki kadi
hizo za benki,ni kinyume cha sheria na kuwa jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi zaidi
ambapo pindi ukikamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara moja.
Katika hatua nyingine,jeshi hilo
linawashikilia watu wawili wakazi wa kijiji cha Runzewe wilayani
Chato,wakituhumiwa kutaka kumuua kwa kumkata mapanga mkazi mmoja wa kijiji
hicho kwa kinachodhaniwa ni ugomvi wa shamba.
Kamanda wa polisi mkoani Geita,Leonard Paulo,aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bw.Marco Mathias (46) na Bw.Boniphace Shija (33) wote wakazi wa kijiji hicho na kuwa tukio hilo lilitokea juzi.
-majira