HII ni miaka minne iliyopita. Lakini, madhara yake yatadumu miaka na miaka. Kwa sababu hii inahusu ujumbe mfupi wa maneno aliyotuma staa wa Kiargentina Lionel Messi kwenye simu ya Mhispaniola Pep Guardiola. Unajua ilikuwaje?
Mambo yalivyokuwa
Lionel Messi alikuwa na hasira, amenuna. Wakati
huo wakiwa ndani ya basi wakitoka kwenye mechi. Messi aliketi siti ya
nyuma tu kutoka alipokuwa amekaa Guardiola.
Kocha Guardiola ndiye aliyesababisha hasira hizo
za Messi. Guardiola simu yake hakuwa ameweka mlio, alitumia mtetemo
(vibration) kutambua simu na meseji zinazoingia.
Mara simu ya Pep ikawa kwenye mtetemo kuashiria
kuna meseji imeingia. Hakuijali na aliendelea kutazama kitu kwenye
skrini ndogo ya televisheni iliyokuwa ndani ya basi hilo.
Pep afungua meseji kuisoma
Kitu cha kwanza kufanya Guardiola, alishangaa.
Alimnong’oneza swahiba wake aliyekuwa ameketi pembeni, Manel Estiarte
na kumwambia: “Tazama hii.”
Wote walishangaa kuona meseji hiyo ilikuwa inatoka
kwa Messi. Meseji ya Muargentina huyo ilimweka majaribuni kocha wake
hasa baada ya kufanya usajili wa straika Zlatan Ibrahimovic kwenye
majira ya kiangazi mwaka 2009, wakati tukio lenyewe lilitokea majira ya
kipupwe mwaka huo.
Meseji yenyewe ilisomeka hivi: “Sawa, najua sina umuhimu tena kwenye timu, hivyo...”
Messi alijificha kwenye vitufe vya simu, hakuwa
mbali na alipoketi lakini aliona njia pekee ya kumweleza jambo Guardiola
ni kumtumia ujumbe mfupi wa maneno. Mwanasoka huyo bora wa dunia mara
nne hakuwa mtu wa maneno mengi, hivyo alitumia meseji kufanya
mawasiliano kuliko kuzungumza ana kwa ana.
Kilichosababisha tukio
Kuwasili kwa Zlatan Ibrahimovic, mchezaji ambaye Guardiola
alifanya kazi kubwa kumsajili, liligeuka kuwa tatizo kubwa kwa Lionel
Messi. Jambo hilo aligundua kwamba linafuta umaarufu wake kwenye kikosi
cha Barcelona, hivyo aliamua kupambana mapema ili kulinda hadhi yake.
Zlatan kwa kuwa kwenye kikosi hicho kulimvuruga zaidi Messi na hivyo
kuharakisha kuweka mambo sawa mapema kabla ya kuchelewa. Lakini, meseji
yake hiyo moja ilibadili kila kitu na Zlatan akaonekana hana nafasi tena
na Messi alishinda vita.
Kilichoibuka vyumbani
Habari za kwamba Messi alimtumia ujumbe mfupi wa
maneno Guardiola kulalamikia nafasi yake kwenye timu zilivuja na kuwa
gumzo kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Kuna wachezaji hawakupendezwa na jambo hilo na kumtafsiri mchezaji huyo kwamba ni mbinafsi.
Vyumbani kukawa na maneno ya chini chini kuhusu
Messi na sakata hilo ndilo lililomfanya Ibrahimovic kuondoka kwenye timu
hiyo na kutangaza uadui dhidi ya Guardiola na Messi.
“Messi si kama ni dikteta, lakini amekuwa akifanya
mambo kwa kujifikiria yeye binafsi na kutaka kuhodhi kila kitu,”
alisema mmoja wa wachezaji kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo
Nou Camp.