Like Us On Facebook

Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam yawaachia HURU wafuasi wa Sheik Ponda

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetengua adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Machi 21 mwaka huu, dhidi ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda Issa Ponda  kwa sababu adhabu hiyo ilitolewa kinyume na sheria husika.

Hukumu ya Rufaa hiyo imetolewa asubuhi na Jaji Salvatory Bongole ambaye alisema  Agosti 12 mwaka huu alisikiliza  hoja za wakili wa waomba rufaa (Mohamed Tibanyendera) na hoja zilizotolewa na mawakili wa Serikali, Peter Njike ambapo Wakili Tibanyendera alichambua kosa la kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya 
mwaka 2002, kosa la pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha sheria hiyo  ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002.

"Kwa masikitiko makubwa tu  nasema kosa la kula njama halikuthibitika, na hakimu Fimbo alikosea kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama kwa kutumia kifungu hicho cha 384 cha sheria ya Kanuni ya adhabu. 

"Na, kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002, inasema wazi kabisa mtu anayekutwa na hatia ya kutenda kosa la mkusanyiko haramu atapaswa alipe faini ya Sh.50,000 au kwenda jela miezi mitatu au vyote pamoja. Lakini tunashangaa huyu hakimu Fimbo ametoa adhabu ya juu kabisa ya mwaka mmoja jela. 

Sijui hiyo sheria ameipata wapi? Tunaomba mahakama hii itengue hukumu hiyo kwani ina dosari nyingi za kisheria na hakukuwa na ushahidi wowote wakuweza kuishawishi mahakama hiyo iwatie hatiani waomba rufaa,” alidai wakili Tibanyendera.

Kwa upande wake wakili wa serikali, Njike aliiomba mahakama isitengue hukumu hiyo kwa sababu hukumu ile ya Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi kisheria na kwamba upande wa Jamhuri ulileta ushahidi mzito ambao uliishawishi mahakama ya Kisutu kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa matatu ya kula njama, kufanya maandamano haramu na kukaidi amri ya jeshi la Polisi.

Akitoa hukumu ya Rufaa hiyo, Jaji  Bongole alisema anakubaliana na wakili wa waomba rufaa kuwa hakimu Fimbo alikosoea kuwatia hatiani katika kosa la kwanza la kula njama, kwani hakukuwepo na ushahidi unaonyesha washitakiwa walitenda kosa hilo la kuja njama kutenda kosa hivyo mahakama yake inawaachiria huru washitakiwa hao katika kosa hilo la kwanza la kula njama kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani.

Aidha, Jaji Bongole alisema hakubaliani  na ombi la waomba rufaa lililotaka mahakama iwaachiriwe katika kosa la pili la kufanya maandamano haramu kwenda katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk Eliezer Feleshi kushinikiza DPP amwachirie huru Ponda aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa malighafi na uchochezi katika Mahahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambayo ilimhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja.

“Mahakama hii imekataa kuwaachiria huru katika kosa la pili la kufanya maandamano haramu kwenda ofisi ya DPP na pia imekataa kuwaachiria huru katika kosa la tatu na kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike kwasababu, upande wa Jamhuri uliweza kuleta ushahidi ambao umedhibitisha waomba rufaa walitenda makosa hayo mawili. 


"Mahakama Kuu inawatia hatiani kwa makosa hayo na Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi kuwatia hatiani katika makosa hayo,” alisema Jaji Bongole.

Hata hivyo Jaji Bongole alisema pamoja na mahakama yake kuwatia hatiani katika makosa hayo mawili, ambapo kwa mujibu wa Sheria ya polisi, mtu anayepatikana na hatia katika makosa hayo anapewa adhabu ya  ya kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela na faini ya Sh. 50,000 na kwamba mahakama yake inawapatia adhabu hiyo  kwa sababu ndiyo adhabu iliyowekwa na Sheria ya Jeshi la Polisi hivyo hakimu wa Mahakama ya Kisutu alikosoea kuwapatia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja.

Aidha, Jaji Bongole alisema licha ya mahakama yake kuwapatia adhabu hiyo, pia mahakama yake imeona washitakiwa ambao walikuwa wakitumikia adhabu ya mwaka mmoja gerezani tayari wameishakaa gerezani muda mrefu na adhabu ya kisheria kwa mujibu wa makosa hayo ya miezi mitatu imeishapita, hivyo mahakama yake inawaachiria huru ila kama waomba rufaa hao wanakesi nyingine, waendelee kushikiliwa na mamlaka nyingine.

Hata hivyo, mwandishi wetu  saa nne asubuhi alishuhudia waomba rufaa hao wakipakizwa kwenye basi la jeshi la Magereza na kurudishwa gerezani hadi pale mahakama itakapopeleka hati inayoonyesha waomba rufaa hao wameachiwa na Mahakama hiyo. Ulinzi ulikuwa umeimarishwa na hapakuwepo na vurugu zozote.

Kesi hiyo ilifunguliwa  rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,  Februali 18 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, na siku hiyo hiyo upande wa Jamhuri ukasema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. 


Februali 19 mwaka huu, upande wa Jamhuri uliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao na shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alianza kutoa ushahidi wake hadi Februali 26 mwaka huu. 

Upande wa Jamhuri ulifunga ushahidi wake. Washitakiwa walianza kujitetea Februali 19 mwaka huu. Machi 21 mwaka huu, Mahakama hiyo ilimaliza kusikiliza kesi hiyo kwa kutoka hukumu yake ambapo iliwahukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa makosa ya kula njama, kufanya maandamano haramu na kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 22 mwaka 2013.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari