Alisema kuwa kwa sasa chama hicho kikongwe kimepoteza matumaini kwa Watanzania kutokana na vitendo ambavyo siyo vya kiungwana vinavyofanywa na watendaji.
Kwa kusisitiza, Kikwete alisema hata kama CCM itashinda uchaguzi wa 2015, kama tabia walizonazo watumishi na viongozi ndani ya chama hazitabadilika, ni wazi kuwa hakitapita kwenye uchaguzi wa 2020.
Rais Kikwete alitoa onyo hilo mjini Dodoma juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa wa chama hicho nchini nzima.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana, na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea sh laki mbili za ‘airtime’ (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika, ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema.
Alisema tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu, nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali nawaambieni,” alisema Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga mafunzo hayo.
Alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama ubunge.
Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.
Akizungumzia chuki ndani ya chama, alisema Watanzania kwa sasa wameishakuwa na akili zao, na hivyo hawataki kudanganywa kwani viongozi wengi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama chao.
“Wapo baadhi ya viongozi ndani ya chama hawajui hata ilani ya chama chao, wakipanda kwenye majukwaa wanaanza kuzungumzia ujenzi wa daraja la Mkapa ama lile la Malagarasi, watu hawataki kusikia hayo, mtu wa Ngara anataka kujua daraja lake limeishaje siyo la Mkapa,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa vyama vya upinzani vinafanya kazi kubwa zaidi ya kuwatembelea wananchi na kusikiliza kero zao tofauti na ilivyo kwa CCM ambayo viongozi wake wapo mbali na wananchi.
“Wapo watu ambao wanadai kuwa chama kitafia mikononi mwangu, nataka niseme kuwa hakifii mikononi mwangu, kitafia mikononi mwenu,” alisisitiza.
Kikwete alisema kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao, na hivyo kuwataka viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi zao.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi. Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”alisema.
Katika hatua nyingine, Kikwete aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta wengine wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
-Tanzania dai