Mwili wa mtangazaji mkongwe, Julius Masyaga Nyaisanga maarufu kama ‘Uncle J’ (53), aliyefariki dunia Jumapili iliyopita katika Hospitali ya Mazimbu mkoani Morogoro, unatarajiwa kuletwa leo jijini Dar es Salaam na baadaye kuagwa kwenye Viwanja vya Leaders’ Club.
Meneja Matangazo wa Kituo cha Abood Media, Abeid
Dogoli alisema mwili wa Nyaisanga uliagwa jana jioni mjini Morogoro na
leo alfajiri unasafirishwa kuja Dar es Salaam.
“Mwili wa marehemu utaagwa kesho (leo) kwenye
Viwanja vya Leaders, na shughuli zitaanza saa 4 asubuhi baada ya kutoka
Hospitali ya Taifa, Muhimbili,” alisema rafiki wa karibu wa marehemu,
Aboubakar Liongo.
Liongo aliyewahi kufanya kazi pamoja na Nyaisanga
wakati huo ikijulikana kama Radio Tanzania (RTD) na baadaye Radio One,
alisema baada ya shughuli ya kuaga, mwili wake utapelekwa Uwanja wa
Ndege wa Julius Nyerere tayari kwa safari ya kwenda Mara kwa mazishi.
Mkoani Morogoro, mwili uliagwa nyumbani kwake eneo
la Kihonda Viwandani, na mke wake Leah Nyaisanga alisema wamepanga
kuondoka Jumanne kwenda Tarime.
Nyaisanga alifariki dunia katika Hospitali ya
Mazimbu inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), siku
moja baada ya kufikishwa na kulazwa kutokana na maradhi ya ugonjwa wa
kisukari.
Wakati huohuo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Nyaisanga.
Nyaisanga pia aliyewahi kufanya kazi Radio
Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo hivi sasa ni TBC Taifa na katika
Kampuni ya IPP, ambako alikuwa Mkurugenzi wa Radio One.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa
kutokana na kifo cha mtangazaji maarufu na mkongwe hapa nchini katika
Tasnia ya Habari hususan upande wa Utangazaji, Julius Nyaisanga kwani
kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa katika Tasnia hiyo”, alisema Rais
Kikwete katika salamu zake.
Nyaisanga aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Abood, ameacha mjane na watoto wawili wa kike, Boke na Nyange.