Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutokutajwa jina, mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo, alisema kwa
kawaida upasuaji kama huo ukifanyika kinachokuwa kinasubiriwa ni mgonjwa
kupona vidonda au kupungua kwa maumivu kabla ya kuruhusiwa.
“Kimsingi hadi kufanyiwa upasuaji wa namna hiyo ni
kuwa ameshatoka katika ile hali ya hatari na ameshasafishwa na
kuondolewa uchafu wote uliokuwepo ikiwa ni pamoja na kumtibia vidonda
vilivyotokana na shambulizi hilo,” alisema daktari huyo.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Aminiel Eligaeshi alisema Ufoo anaendelea vizuri na hivi sasa ameanza
kula, kufanya mazoezi kidogo na kujaribu kuzungumza, lakini bado
hajaruhusiwa kukutana na watu zaidi ya ndugu wachache ambao pia
wanamwangalia kwa karibu.
Msemaji wa familia ya Ufoo, Allelio Swai
alithibitisha kutengemaa kwa hali ya mwandishi huyo.Swai alisema Ufoo
hivi sasa anaendelea vizuri na madaktari wamewaeleza kuwa wakati wowote
anaweza akaruhusiwa.