Like Us On Facebook

WANAOWAPA HIFADHI WAHAMIAJI HARAMU MIPAKANI SASA KUFILISIWA MALI ZAO

           WAKATI msako mkali ukiendelea dhidi ya wahamiaji haramu waliokataa agizo la Serikali la kurejea katika nchi zao bila shuruti, Idara ya Uhamiaji imesema sheria inaruhusu kutaifishwa kwa mali za wanaosaidia wahamiaji haramu kusafiri au kuishi nchini.
Mali hizo ni pamoja na nyumba na magari. Tayari nyumba mbili wilayani Hai na Rombo, pikipiki moja na gari vimewekwa chini ya ulinzi ili kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kujiridhisha jinsi zilivyotumika kuhifadhi na kusafirisha wahamiaji haramu na ikithibitika zitataifishwa.
Hayo yalithibitishwa jana na Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kilimanjaro, Johanes Msumule katika mahojiano maalumu na gazeti hili, kuhusu jitihada za kudhibiti wahamiaji haramu ambao wanatumia wilaya hizo kama njia kuu za kufanikisha safari zao.
“Kwa mujibu wa sheria, ikithibitika nyumba, gari au mali yoyote kuhusika kusaidia wahamiaji haramu kuwasafirisha au kuwahifadhi, itataifishwa huku mtuhumiwa husika akistahiki kifungo kulingana na matakwa ya sheria,” alisema.
Kadhalika, ofisa huyo alisema mkoa umepunguza wimbi la wahamiaji haramu wanaoingia nchini ambapo kati ya Januari na Julai wamekamata wahamiaji 471 huku kipindi kama hicho mwaka jana wakikamata wahamiaji 609.
Pamoja na hilo, Idara hiyo imerejesha kwao wahamiaji 368, kushitaki 156, kufunga gerezani 103 na 27 kutozwa faini kwa viwango tofauti.
Msumule alisema kutokana na uchunguzi wa maofisa wa idara hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola, Watanzania watano wameshitakiwa na kesi zao zinaendelea mahakamani kwa tuhuma za kusaidia wahamiaji hao kuingia nchini.
Ofisa huyo alisema Idara imejiwekea lengo la kukutana na makundi muhimu katika jamii ili kuwaelimisha majukumu yake na kueleza changamoto na mafanikio yake ili kuomba ushirikiano katika kudhibiti wimbi la wahamiaji hao.
Alisema tayari wamefanya kikao na walimu na wamiliki wa shule binafsi na vyuo mkoani humo, ambapo waliombwa kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wahamiaji hao hawaingii wala kuajiriwa katika taasisi hizo.
Msumule alisema Oktoba 3 Idara itafanya mazungumzo na wamiliki wa hoteli, nyumba za kulala wageni na sekta zingine binafsi ili kupokea maoni yao, lakini pia kuisaidia kukabili wimbi hilo.
Wakati huo huo,Watanzania 60 wamefungwa katika magereza nchini Kenya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kwa kuingia na kuishi nchini humo kinyume cha sheria.
Hayo yalielezwa na Msumule ambaye alisema Watanzania hao ambao baadhi ni wafanyabiashara wanaotumia mipaka ya Holili na Tarakea wilayani hapa, walihukumiwa kwa nyakati tofauti baada ya kupatikana na hatia ya kuingia nchini humo ama kwa ‘njia za panya’ au biashara.
Ofisa Uhamiaji Mfawidhi Kituo cha Holili, Fredrick Kiondo alikiri kupokea malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara ndogo wa Tanzania kufungwa Kenya, huku wengine wakilalamikia mazingira ya biashara nchini humo kuwa magumu.
“Ni kweli wafanyabiashara wa Tanzania wanaokwenda Kenya wanalalamikia mazingira yasiyo sawa baina ya nchi hizi mbili, wanasema wakati Wakenya wanaruhusiwa kuingia nchini umbali wa kilometa 12 na kupata huduma na biashara, kwa Kenya, umbali kama huo kutoka mpakani ni pori na hakuna huduma,” alisema.
Alisema kutokana na mazingira hayo, wafanyabiashara wa Tanzania wanalazimika kuingia umbali unaozidi kilometa 12 hadi Taveta, jambo linalosababisha kuonekana wameingia nchini humo kinyume cha sheria na kukamatwa na kukabiliwa na adhabu kikiwamo kifungo gerezani.
Ili kukabiliana na kilio hicho, Kiondo alisema walifanya vikao vya ujirani mwema na kuelimisha askari wa Kenya ili kuelewa dhana na ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuonesha mafanikio ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja, idadi ya Watanzania waliokutwa na makosa ya uhamiaji ilipungua na kufikia watano.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari