MV Gold Star ikiungua baada ya kuchomwa moto na wasafirishaji wa madawa ya kulevya.
-NI MV GOLD STAR-WATUHUMIWA WAICHOMA MOTO KUPOTEZA USHAHIDI, WAJITOSA MAJINI
-ILIKUWA NA DAWA ZA KULEVYA ZENYE THAMANI YA BILIONI 126.5
-MZIGO ULIOKUWEMO NI TANI 30 ZILIZOKUWA ZINAPELEKWA UTURUKI
-9 WAKAMATWA, NI RAIA WA MISRI NA SYRIA
MELI iliyosajiliwa nchini Tanzania ya MV Gold Star imekamatwa nchini Italia ikiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya pauni milioni 50 sawa na shilingi bilioni 126. 5. Watuhumiwa waliokuwa ndani ya meli hiyo waliamua kuichoma moto ili kupoteza ushahidi na kuamua kupiga mbizi majini lakini walitiwa nguvuni na wanausalama wa Italia.
Meli hiyo ya mizigo ilikuwa imepakia tani 30 za madawa na ilikamatwa jirani na Kisiwa cha Sicilia katika Bahari ya Mediterranian nchini Italia wakati ikielekea Uturuki. Maofisa wa polisi nchini humo wamedai kuwa watuhumiwa tisa waliokamatwa ni raia wa Misri na Syria na watafikishwa mbele ya sheria. Moto katika meli hiyo umezimwa na tayari imepelekwa katika Bandari ya Sicilia.