Like Us On Facebook

KIONGOZI WA UAMSHO SASA MAHUTUTI HOSPITALI

Kiongozi mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu,Sheikh Khalid Azzan Hamdan amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza na polisi kuanzia Septemba Mosi mjini hapa imefahamika. 

Akizungumza na Mwananchi Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza), Khalifa Hassan alisema Azzan aliwahi kuishiwa nguvu za miguu mara mbili akiwa katika mahabusu ya Gereza la Kinuai,Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.
Hassan alisema,kufuatia hali hiyo, magereza waliamua kumpelekea katika hospitali hiyo ya Mnazi Mmoja na kuamriwa alazwe kwa uchunguzi zaidi na matibabu kufuatia afya yake kuzorota ghafla. Alisema, watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi ya uharibifu wa mali na kuhatarisha usalama wa Taifa mbali na Azzan, wanaendelea vizuri na wako katika afya njema ambapo jana walifikishwa mahakamani bila ya mshtakiwa mwenzao huyo kuwapo.
Wakili wa washtakiwa hao, Abdallah Juma alisema baada ya kupokea taarifa za mteja wake kuwa mgonjwa, aliamua kumjulia hali akiwa hospitali, lakini askari walioimarisha ulinzi katika chumba cha wagonjwa wa mahabusu na wafungwa walisema hawawezi kumruhusu bila ya kupewa kibali cha uongozi wa magereza Zanzibar.
Hata hivyo, Wakili Abdallah alisema, mteja wake Azzan anasumbuliwa na matatizo katika kibofu cha mkojo kutokana na kuwa na vijiwe ambapo alitakiwa kutibiwa nchini India na Afrika Kusini.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,Omar Abadllah Ali alisema kwamba tayari daktari anayemshughulikia ameshachukua vipimo muhimu na anaendelea kufanya vipimo maalumu kwa kutumia mashine ya picha.
Hata hivyo alisema ni mapema kuyazungumzia maradhi yanayomsumbua mtuhumiwa huyo, lakini alikiri na kusema amelezwa katika chumba maalumu hospitalini hapo.

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari